Wizara ya Afya imeungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Magonjwa Adimu Duniani leo Februari 28, 2026, kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu changamoto zinazowakabili wagonjwa na familia zao. Duniani kote kuna takribani magonjwa adimu 7,000, ambayo huathiri idadi ndogo sana ya watu, ambapo kwa wastani ni watu 10 kati ya 10,000 pekee wanaoweza kuugua. Maadhimisho haya yanalenga kuhamasisha jamii, wataalamu wa afya na wadau mbalimbali kushirikiana katika kuboresha utambuzi, matibabu na msaada kwa waathirika.
Magonjwa adimu ni yale yanayowapata watu wachache sana katika jamii, lakini athari zake kwa maisha ya mgonjwa huwa kubwa. Mifano ya magonjwa hayo ni pamoja na Huntington’s disease, Muscular dystrophy, Thalassemia na Crohn’s disease. Magonjwa mengi adimu husababishwa na hitilafu katika vinasaba (genes), hivyo kuhitaji uchunguzi wa kitaalamu na ufuatiliaji wa karibu kwa muda mrefu.
Kupitia maadhimisho haya, Wizara ya Afya imehimiza jamii kutowabagua wala kuwanyanyapaa waathirika wa magonjwa adimu, bali kuwapa ushirikiano na msaada unaohitajika. Pia imeeleza umuhimu wa kufanya uchunguzi wa mapema na kupata ushauri wa kitaalamu pindi dalili zinapoonekana, ili kuongeza nafasi ya kupata matibabu stahiki na kuboresha ubora wa maisha ya wagonjwa.


Hakuna maoni:
Chapisha Maoni