Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) – Mloganzila kwa kushirikiana na Taasisi ya Vision Care imehitimisha kambi maalum ya uchunguzi na matibabu ya kibingwa ya macho kwa wananchi 480 wa Wilaya ya Kisarawe mkoa wa Pwani iliyofanyika kwa siku tatu kuanzia Machi 24 hadi 26, 2026 katika Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe.
Kambi hiyo imehusisha utoaji wa huduma mbalimbali ikiwemo uchunguzi wa macho, matibabu, utoaji wa dawa, miwani pamoja na upasuaji kwa wagonjwa waliobainika kuwa na matatizo makubwa ya macho.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha kambi hiyo, Dkt. Audrey Mwashilemo, Bingwa wa Magonjwa ya Macho MNH Mloganzila, amesema wagonjwa 15 wamefanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho huku wengine wakifanyiwa upasuaji mwingine wa macho.
Ameongeza kuwa magonjwa yaliyoongoza kwa wakazi wengi waliopatiwa huduma ni pamoja na presha ya macho, kushindwa kuona mbali na kushindwa kuona karibu, hali inayoonesha uhitaji mkubwa wa huduma za macho katika jamii.
“Tunawapongeza wananchi wa Kisarawe kwa mwitikio mkubwa wa kujitokeza kupata huduma. Hii ni hatua muhimu katika kuhakikisha wanapata matibabu mapema na kuzuia madhara makubwa ikiwemo upofu,” amesema Dkt. Mwashilemo.
Aidha, baadhi ya wananchi walionufaika na huduma hizo wameishukuru MNH Mloganzila pamoja na washirika wake kwa kusogeza huduma karibu na jamii, wakieleza kuwa imepunguza gharama na muda wa kusafiri kwenda kutafuta matibabu katika hospitali za mbali.
Kambi hiyo imefanyika kwa ushirikiano na Vision Care, Shirika la Msaada la Kimataifa linalojishughulisha na kuzuia upofu duniani, kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Korea Kusini (KOICA), ambapo tangu mwaka 2020 limekuwa likishirikiana na MNH Mloganzila pamoja na wilaya sita za Mkoa wa Pwani kuboresha huduma za macho.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni