Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania imetoa angalizo la uwezekano wa vipindi vifupi vya mvua kubwa kunyesha katika baadhi ya mikoa ikiwemo Lindi, Mtwara, Ruvuma, Morogoro, Mbeya, Iringa, Njombe, Dodoma na Singida ndani ya saa 24 zijazo kuanzia saa 3:00 usiku wa leo Machi 14, 2026. Kwa mujibu wa utabiri huo, maeneo mengi ya nchi yanatarajiwa kuwa na hali ya mawingu, mvua pamoja na ngurumo katika maeneo machache huku kukiwa na vipindi vya jua.
Kwa upande wa ukanda wa pwani na visiwani, mikoa ya Tanga, Dar es Salaam pamoja na Mkoa wa Pwani ikijumuisha visiwa vya Mafia, na visiwa vya Unguja na Pemba inatarajiwa kuwa na hali ya mawingu kiasi, mvua katika maeneo machache na vipindi vya jua. Hali kama hiyo pia inatarajiwa katika mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Mara na Simiyu pamoja na maeneo ya kanda ya kati na magharibi mwa nchi.
Aidha, viwango vya joto vinatarajiwa kutofautiana katika miji mbalimbali ambapo Dar es Salaam na Tanga zinatarajiwa kufikia nyuzi joto 31°C kwa kiwango cha juu, huku Mbeya ikitarajiwa kuwa na kiwango cha juu cha nyuzi 24°C. Upepo wa pwani unatarajiwa kuvuma kutoka Kaskazini Mashariki kwa kasi ya kilomita 30 kwa saa katika pwani ya kaskazini na kilomita 20 kwa saa katika pwani ya kusini, huku hali ya bahari ikitarajiwa kuwa na mawimbi madogo hadi makubwa kiasi. Mamlaka hiyo imeeleza pia kuwa matarajio ya siku ya Jumatatu Machi 16, 2026 ni kuendelea kwa vipindi vya mvua katika maeneo mengi ya nchi.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni