Breaking


Jumatatu, 16 Machi 2026

DARAJA MKUYUNI LIMEANZA ‘KULIPA’ - ULEGA


Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema kukamilika kwa ujenzi wa daraja la Mkuyuni jijini Mwanza, tayari kumeanza kuonesha matunda katika siku zake za awali.

Akizungumza na wananchi baada ya ukaguzi wa daraja hilo, Waziri Ulega, amesema wakazi wa Mwanza ni mashahidi wa hali hiyo hasa kufuatia matukio ya karibuni ya mvua kubwa zilizonyesha, ambapo kama kusingekuwa na daraja, maafa makubwa yangetokea.

Daraja hilo ambalo ujenzi wake ulianza mwezi Novemba mwaka 2024 na kugharimu zaidi ya shilingi Bilioni-5, ni sehemu ya miradi ya dharura 81 ambayo Rais Dokta Samia Suluhu Hassan, aliagiza ijengwe kwa thamani ya zaidi ya shilingi Bilioni-560 ili kuboresha miundombinu iliyoathiriwa na mvua na vimbunga miaka miwili iliyopita. 

Waziri Ulega, ametembelea daraja hilo ikiwa ni sehemu ya maelekezo aliyopewa na Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba, kuhakikisha ujenzi wake unakamilika haraka ili kuondoa usumbufu kwa wananchi.

Baada ya ukaguzi huo, amesema atafikisha salamu kwa Waziri Mkuu kuwa kazi hiyo iliyofanywa na mkandarasi mzalendo wa kampuni ya JASCO sasa imekamilika rasmi, ikiwemo ufungwaji wa taa za barabarani.

Akitoa taarifa kuhusu daraja hilo, Meneja wa TANROADs, Mkoa wa Mwanza, Paschal Ambrose, amesema daraja hilo lina upana wa mita 15 na njia sita-nne za magari na mbili za watembea kwa miguu. 

Kukamilika kwa daraja hilo kutafungua zaidi njia ya usafiri wa barabara kati ya mikoa ya Mwanza na Shinyanga na kwamba itakuwa na msaada mkubwa hasa katika nyakati za masika ambako eneo la Mkuyuni lilikuwa likifahamika kwa kutopitika.

Hakuna maoni: