Kituo cha kupoza umeme cha Ifakara, wilayani Kilombero, mkoani Morogoro, kilichotekelezwa na Wakala wa Umeme Vijijini-REA, kilichogharimu shilingi bilioni 25, kimesaidia kuchochea uchumi na maendeleo ukanda wa Morogoro Kusini.
Uwepo wa kituo hicho kinachopokea umeme kutoka bwawa la Kidatu na Kihansi umepongezwa pia na mkuu wa wilaya ya Kilombero, Wakili Danstun Kyobya, huku akitoa wito wa wawekezaji kujitokeza kwa wingi kuwekeza katika wilaya hiyo kwa kuwa ina umeme wa ziada wa kilovoti 11.
Tayari, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imetumia shilingi bilioni 25 kujenga Kituo hicho cha Kupoza Umeme 1x20MVA, 220/33kv pamoja na njia za kusambaza Umeme katika Wilaya ya Kilombero, hatua ambayo imeboresha upatikanaji wa umeme na kuondoa changamoto ya kukatika kwa nishati hiyo katika wilaya za Kilombero, Ulanga na Malinyi.
Hayo yamesemwa wakati wa ziara ya Jukwaa la Wahariri Tanzania-TEF waliotembelea mradi huo kujionea utekelezaji wake na tija yake kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika ukanda wa Morogoro Kusini.
Kuimarika kwa huduma ya umeme kumechochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi, hususan katika sekta za viwanda, uchimbaji madini, kilimo na huduma za kijamii.
Naye, Meneja wa Usimamizi wa Miradi ya Kusambaza Umeme kutoka REA, Deogratius Nagu, amesema gharama za mradi huo zinahusisha pia usimikaji wa mashine umba (transfoma) yenye teknolojia ya nchi tatu pamoja na mifumo yake ya uendeshaji, udhibiti na ulinzi, ujenzi wa njia za kusafirisha umeme za msongo wa kilovolti 33 zenye urefu wa kilometa 70 pamoja na gharama za mshauri elekezi.
Kituo hicho ni cha kisasa, kikiwa na teknolojia kutoka nchi mbalimbali ikiwemo transfoma kutoka Bulgaria, mifumo ya udhibiti na ulinzi kutoka Hispania pamoja na mifumo ya switching (switchgears) kutoka Ujerumani.
Naye, Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, amesema uwekezaji huo unaonesha matumizi sahihi ya rasilimali za umma na mchango wa REA katika kusambaza huduma ya umeme vijijini.
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya wasichana ya Kilimo Ifakara, Setina Ngailo, amesema huduma ya umeme imeimarika na kuondoa changamoto ya kukatika kwa umeme iliyokuwa ikiathiri shughuli za shule.
Naye, Msimamizi wa Hospitali ya Kansa ya Good Samaritan, Father Charles Masawe, amesema upatikanaji wa umeme wa uhakika umeongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za afya kwa kupunguza utegemezi wa jenereta.
Naye Meneja wa Kiwanda cha Kukoboa Mpunga cha Bezelengule, Enos Machumu, amesema uzalishaji umeongezeka kwa kiasi kikubwa kufuatia kuboreshwa kwa huduma ya umeme, hali iliyorejesha wateja na kulinda mitambo dhidi ya uharibifu.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni