Wizara ya Maji imetangaza kufanyika kwa mkutano wa mwaka wa usalama wa mabwawa utakaofanyika jijini Mwanza kuanzia Oktoba 21 hadi 23, 2026, ukiwa na lengo la kuimarisha usimamizi na usalama wa miundombinu ya mabwawa ya maji na tope sumu nchini kuanzia hatua ya usanifu, matumizi hadi ufungaji.
Akizungumza na waandishi wa habari Machi 31, 2026 jijini Dodoma, mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Robert Sunday amesema mkutano huo unaandaliwa kwa ushirikiano na Chemba ya Migodi Tanzania pamoja na Kampuni ya City Engineering, ukilenga kuwakutanisha wadau mbalimbali kujadili masuala ya usalama wa mabwawa.
Amesema Sera ya Taifa ya Maji ya mwaka 2002 toleo la 2025 imeweka msisitizo katika uendelezaji wa rasilimali za maji ili kuhakikisha usalama wa maji, chakula na kukuza uchumi sambamba na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Amesema Wizara ya Maji kupitia Idara ya Rasilimali za Maji ina jukumu la kuhakikisha mabwawa yote yanazingatia viwango vya usalama kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizopo, huku ikiendelea kutoa elimu kwa wadau ili kuongeza uelewa wa masuala ya usalama.
Amesisitiza kuwa mabwawa yana muda maalum wa matumizi, hivyo ni muhimu kuyasimamia kwa kuzingatia mzunguko wake wote ili kuongeza uhai na kuhakikisha usalama wake kwa muda mrefu na kutoa wito kwa wadau wote kujisajili kushiriki katika mkutano huo kupitia tovuti maalum, akibainisha kuwa ushiriki wao ni muhimu katika kulinda rasilimali za maji na mazingira.
Naye Mkuu wa Kitengo Cha Usalama wa Mabwawa,DOmina Msonge amesema tope simu ni tope linalotokana na uchenjuaji wa Madini huku akisisitiza kuwa hali ya Mabwawa ya tope sumu hapa nchini iko salama.
Awali Mkurugenzi mtendaji Kampuni ya City Engineering Anael Macha, amesema mkutano huo unatarajia kushirikisha zaidi ya washiriki 200 ukiwa unakuja wakati Tanzania inaelekea mbele kwa nguvu chini ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, na wanatengemea kuungwa mkono na wa makampuni ya Madini, taasisi za fedha, wasbazaji wa vifaa vya uhandisi na washiriki wote wa sekta binafsi



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni