Wanafunzi 725 wa Shule ya Msingi Butimba A na B, mkoani Mwanza, wamepata mafunzo ya huduma ya kwanza kwa mtu aliyezama Maji.
Mafunzo hayo yametolewa na Chuo Cha Polisi Wanamaji Tanzania, kilichopo mkoani Mwanza ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kutoa elimu kwa makundi mbalimbali katika jamii.
Akiongoza mafunzo hayo, ASP Kagemula Muhula, amesema lengo ni kuwajengea wanafunzi uelewa wa namna ya kukabiliana na majanga, hasa ajali za majini, na kuwapa maarifa ya kutoa msaada wa haraka kabla ya wahudumu wa afya kufika.
Mbali na mafunzo ya nadharia, wanafunzi pia walioneshwa vifaa vya uokozi majini ili kuvitambua na kuelewa matumizi yake wakati wa dharura.
Walimu pamoja na wanafunzi walitoa shukrani za dhati kwa chuo hicho kwa kuwafikia na kuwapatia elimu muhimu itakayosaidia kuokoa maisha katika jamii. Mafunzo hayo yamewajengea ujasiri, maarifa na utayari wa kuchukua hatua sahihi pindi majanga yanapotokea.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni