Breaking


Jumamosi, 21 Machi 2026

RAIS DKT SAMIA AOMBOLEZA KIFO CHA MWANASHERIA NGULI JULIE MANNING


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha aliyewahi kuwa Waziri wa Sheria, Julie Manning, akieleza kupokea kwa masikitiko makubwa taarifa hiyo. Rais Samia amemtaja marehemu kama kiongozi aliyetoa mchango mkubwa katika sekta ya sheria nchini, huku akisisitiza historia yake ya kipekee kama mwanamke wa kwanza Tanzania kusoma Shahada ya Sheria na pia kuwa Jaji wa kwanza mwanamke katika Mahakama Kuu kwa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.


Katika salamu zake, Rais Samia amesema taifa litamkumbuka Julie Manning kwa heshima kubwa kutokana na utumishi wake uliotukuka na mchango wake katika kuimarisha utawala bora pamoja na maendeleo ya sekta ya sheria. Ameongeza kuwa marehemu alikuwa chachu ya mabadiliko hasa katika kuwainua wanawake, akitumia nafasi zake kuhamasisha usawa wa kijinsia na kuwapa wanawake ujasiri wa kufikia ndoto zao katika taaluma mbalimbali.


Aidha, Rais Samia ametoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu pamoja na Watanzania wote walioguswa na msiba huo. Amehitimisha kwa kumuombea marehemu apumzike kwa amani, akisema kuwa mchango wake utaendelea kuishi katika historia ya taifa na mioyo ya wengi walioguswa na maisha na kazi zake.


Hakuna maoni: