Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeweka mazingira rafiki katika sekta binafsi ili kuimarisha vivutio vya uwekezaji, kukuza ushirikiano kupitia ubia wa sekta ya umma na binafsi-PPP katika miradi ya kimkakati.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu siku 100 za mafanikio ya uongozi wa Rais Dokta Hussein Ali Mwinyi, Waziri wa Kazi na Uwekezaji, Shariff Ali Shariff, amesema serikali imetekeleza miradi ya kimkakati ikiwemo miundombinu, nishati mbadala na huduma za kijamii ili kuimarisha uchumi na ukuaji wa nchi.
Aidha, amesema Serikali inaendelea kuratibu program za kusimamia usalama na afya kazini, utekelezaji wa viwango vya kazi ili kulinda maslahi ya wafanyakazi ikiwemo mikataba, mishahara, saa za kazi na stahiki za wafanyakazi.
Waziri Shariff ameeleza kuwa Serikali inaendelea ujenzi wa miundombinu katika maeneo huru ya uwekezaji, ambapo Mamlaka imefanya ukaguzi na tathmini kwa ajili ya ulipaji fidia katika maeneo makuu matatu, ambapo ni tathmini ya upanuzi katika eneo la bandari ya Fumba, ujenzi wa kilometa 8 za barabara za ndani katika eneo la uwekezaji Fumba na eneo la mradi wa IT Madrasa.
Kwa upande wa sekta ya kazi, amesema Kamisheni ya Kazi imefanya ukaguzi wa kawaida kwa taasisi 78 Unguja na Pemba kwa lengo la kuhakikisha zinatekeleza sheria za kazi katika kulinda haki na Maslahi ya wafanyakazi.
Aidha, Waziri Sheriff, amesema Serikali ipo katika hatua ya kufanya tathmini ya kima cha chini cha mshahara kilichopo kwa sasa katika sekta binafsi ambacho kilitangazwa mwaka 2023 kwa lengo la kuangalia uhalisia wake kulingana na mabadiliko ya hali ya uchumi.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni