Breaking


Jumanne, 24 Machi 2026

TANZANIA YAIKARIBISHA AUSTRIA KUONGEZA UWEKEZAJI KUELEKEA DIRA YA 2050

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Dkt. Pius Chaya (Mb), amekaribisha kuimarishwa kwa ushirikiano wa kina kati ya Tanzania na Austria, wenye lengo la kukuza biashara na uwekezaji endelevu kwa manufaa ya pande zote mbili kupitia fursa mbalimbali zilizopo chini ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.

Dkt. Chaya ameyasema hayo tarehe 23 Machi 2026 jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Austria anayeshughulikia masuala ya kisiasa, Mhe. Balozi Dkt. Hannah Liko.

Katika mazungumzo hayo, Dkt. Chaya amewasilisha vipaumbele vya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, inayolenga kuifanya Tanzania kuwa na uchumi wa kipato cha juu unaoongozwa na viwanda, wenye thamani ya takriban Dola za Kimarekani trilioni 1. Amebainisha sekta za kilimo, utalii, viwanda, madini pamoja na uchumi wa bluu zimeainishwa kuwa injini kuu za mageuzi ya kiuchumi.

Aidha, ameeleza kuwa Tanzania inaendelea kujipambanua kama lango la soko la kikanda lenye zaidi ya watu milioni 450, hivyo kuwa kivutio kikubwa kwa wawekezaji kutoka Austria. Ameongeza kuwa ukuaji wa uchumi wa wastani wa asilimia 6.1 kwa kipindi cha miongo miwili iliyopita ni ishara ya uthabiti wa mazingira ya uwekezaji nchini. Sambamba na hilo, amepongeza Mkakati wa Austria kwa Afrika unaolenga kukuza biashara na kuimarisha viwanda vidogo na vya kati (SMEs).

Kwa upande wake, Dkt.Liko ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano mzuri uliopo na kusisitiza umuhimu wa kuzingatia vipaumbele vilivyowekwa katika Mkakati wa Austria kwa Afrika wa mwaka 2026–2029 ili kuimarisha zaidi uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya mataifa hayo mawili.

Kwa mujibu wa Dkt. Chaya, hadi kufikia Februari 2026, takwimu za Mamlaka ya Uwekezaji Tanzania (TISEZA) zinaonesha kuwa jumla ya miradi 17 kutoka Austria imesajiliwa nchini, ikiwa na thamani ya Dola za Kimarekani milioni 36.14, na imezalisha ajira 871 katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, viwanda na nishati.

Hakuna maoni: