Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa, amesema Serikali inaendelea kuwa sikivu kwa kupokea na kuchambua maoni ya wadau wa sekta ya usafirishaji na biashara, akisisitiza kuwa dhamira ya TPA si kuzuia biashara bali kurahisisha na kuwezesha shughuli za kiuchumi. Amesema maoni yote yaliyotolewa yatazingatiwa kwa maslahi mapana ya uchumi wa taifa.
Kauli hiyo imetolewa wakati Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TSPF) kwa kushirikiana na TPA walipoendesha mjadala wa ngazi ya juu wa sekta ya umma na binafsi (PPD – Public-Private Dialogue), uliolenga kujadili utekelezaji wa tozo mpya za bandari za mwaka 2026 katika mazingira ya biashara.
Mjadala huo uliwakutanisha wadau mbalimbali kutoka sekta ya umma na binafsi, wakijadili kwa kina mfumo mpya wa tozo na kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuboresha ushindani wa bandari za Tanzania ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Deogratius Massawe, amesema shirikisho limepokea na kukusanya maoni ya wadau wake kwa umakini, na litaendelea kuyawasilisha kwa mamlaka husika ili kuhakikisha changamoto zinazojitokeza zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati.
Aidha, wadau wamesisitiza umuhimu wa kuongeza ufanisi wa bandari ili ziweze kushindana kikanda na kimataifa, huku wakitaka mfumo wa tozo uwe rafiki kwa biashara na unaozingatia uendelevu. Serikali kupitia TPA imetoa hakikisho kuwa itaendelea kufanyia kazi mapendekezo yote yaliyowasilishwa, na kwamba mrejesho rasmi utatolewa baada ya uchambuzi kukamilika kabla ya kuanza kutekelezwa kwa tozo hizo Julai 1, 2026.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni