Breaking


Ijumaa, 6 Machi 2026

TUIBEBE AGENDA YA MAZINGIRA NA MABADILIKO YA TABIA NCHI PAMOJA.

 


Wadau wa masuala ya Mazingira Nchini , wamekubali kuwa mabalozi wazuri kupitia Jiji la Dar es salaam, kuhakikisha uelewa juu ya utunzaji na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, inakuwa ni agenda ya kudumu.

Kauli hiyo ni matokeo ya darasa la siku mbili, la mabadiliko ya tabia nchi,  lililoandaliwa na taasisi ya C40 cities, kwa kushirikiana na Jiji la Dar es salaam ili kutoa elimu namna ya kufikia malengo juu ya mabadiliko ya tabia nchi.

Akizungumza katika hitimisho la mafunzo hayo, Mkuu wa idara ya Mazingira, halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Theresia Denis, ameeleza ili kufikia malengo ya kuhifadhi mazingira, na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi , wadau wa mazingira ikiwemo serikali, mashirika ya maendeleo kimataifa na  sekta binafsi waungane kufikia malengo. 

Amebainisha kuwa, ili kufikia malengo yote kwa makundi hayo, kila mmoja anatakiwa kuhakikisha kuwa na mipango endelevu na bajeti himilivu ili kufanya shughuli za kimazingira kwa usalama kwa kizazi kilichopo na kijacho.

Ameongeza kuwa, pamoja na bajeti kuzingatiwa, kwa upande mwingine viongozi wa kisiasa bado wananafasi kubwa ya kufikisha ujumbe wa mabadiliko ya tabia nchi kwa jamii wanayoiongoza pamoja na kuipa  nafasi agenda ya mazingira katika vikao vyao vya maamuzi kuanzia ngazi ya chini ambapo kuna shughuli nyingi za uharibifu wa mazingira. 

Theresia, ametumia nafasi hiyo kueleza sababu zinazofanya uharibifu wa mazingira katika shughuli za kila siku kuwa ni uzalishaji taka majumbani, Usafiri na vifaa vya mashuleni, maofisini, na vyuoni. 

Kwa upande wake, Mshauri wa masuala ya mazingira na mabadiliko ya tabia nchi, wa uingereza, nchini Tanzania, Abdallah Shaa, ameeleza suala la nishati safi na taka linatakiwa kuleta mabadiliko ya fursa za ajira badala ya kulalamika.

Amesema katika kujenga uelewa wa pamoja, serikali ya Uingereza ipo tayari kushirikiana na Tanzania, kukabiliana na tabia ya mabadiliko ya tabia nchi. 

Aidha kwa upande wao wadau wengine walioshiriki darasa hilo, wamesema ili kufikia malengo waliyojiwekea ni vema kuimarisha mawasiliano, utafutaji wa fedha, kubadili taka na nishati kuwa fursa ya ajira, kuzifanyia kazi sera zilizopo, kutunza mazingira kwa kurudisha ukijani, kufuata sheria za mipango miji, na kuifanya agenga ya mazingira kuwa muhimu katika vikao.

Darasa la uelewa wa mazingira na mabadiliko ya tabia nchi, limeudhuriwa na wadua wa mazingira kutoka ofisi ya  Mazingira ( NEMC), Ofisi ya Waziri Mkuu, na Makamo wa Rais, Makatibu tawala wa wilaya, Madiwani na wadau wanaobadili taka kuwa nishati safi ya kupikia.

Hakuna maoni: