Breaking


Alhamisi, 9 Aprili 2026

SAMAMBA ATOA WITO GST KUBORESHA MAZINGIRA YA KAZI, KUIMARISHA USHIRIKIANO



Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Eng. Yahya Samamba, ameitaka Menejimenti ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kuhakikisha inajenga mazingira rafiki ya kazi yatakayowawezesha watumishi kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kujisikia salama kazini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Baraza la Wafanyakazi la GST uliofanyika katika ukumbi wa Tume ya Madini jijini Dodoma, Eng. Samamba amesema mazingira bora ya kazi ni msingi muhimu wa kuongeza tija, ubunifu na ufanisi katika utumishi wa umma.

Amesisitiza kuwa watumishi wanapaswa kufanya kazi kwa bidii na ubunifu ili kuiwezesha GST kuwa kitovu cha takwimu za jiosayansi zenye ubora na zinazopatikana kwa urahisi kwa wadau mbalimbali.

“Ni wajibu wa kila mtumishi kutekeleza majukumu aliyopewa kwa weledi na kuchangia kikamilifu mafanikio ya taasisi,” amesema Eng. Samamba.

Aidha, amewataka watumishi kuimarisha mshikamano, umoja na ushirikiano kazini, akibainisha kuwa hali hiyo itaongeza ufanisi katika utoaji wa huduma na kuinua hadhi ya utumishi wa umma.

Katika hatua nyingine, Eng. Samamba amewapongeza viongozi wapya wa Baraza la Wafanyakazi la GST, akieleza kuwa baraza hilo lina jukumu muhimu la kushauri uongozi juu ya ufanisi wa kazi, mipango ya maendeleo, pamoja na kuboresha ustawi wa wafanyakazi.


Amebainisha kuwa majukumu ya baraza yanajumuisha pia kujadili mipango ya mapato na matumizi, kupanga mikakati ya maendeleo ya taasisi, na kuimarisha ushirikiano kati ya wafanyakazi na uongozi.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa GST, Eng. Ally Samaje, amesema taasisi hiyo itaendelea kuboresha utendaji wake ili kuchangia kikamilifu maendeleo ya sekta ya madini nchini.

Ameongeza kuwa GST imejipanga kuboresha huduma zake za jiosayansi na maabara, sambamba na kuendana na mabadiliko ya teknolojia, ili kutoa matokeo yenye tija kwa uchumi wa taifa.

Hakuna maoni: