Breaking


Alhamisi, 5 Machi 2026

USHIRIKIANO IMARA WA MFUKO WA AFYA NI NGUZO YA MAGEUZI YA SEKTA YA AFYA-MCHENGERWA

Waziri wa Afya, Mohammed Mchengerwa, amesema ushirikiano madhubuti kati ya Serikali na Washirika wa Mfuko wa Pamoja wa Afya, umeendelea kuwa chachu ya maboresho makubwa katika utoaji wa huduma za afya nchini.

Akizungumza katika mkutano wa nchi washirika wa Mfuko huo jijini Dar es Salaam, Mchengerwa alianza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuiwezesha Tanzania kufikia hatua ya kufanya majadiliano muhimu kuhusu mustakabali wa sekta ya afya. 

Ameeleza kuwa tangu kuanzishwa kwa Mfuko wa Pamoja wa Afya mwaka 1999, zaidi ya dola za Marekani bilioni 1.3 zimechangishwa kusaidia utekelezaji wa mipango ya kimkakati ya sekta ya afya. 

Asilimia 90 ya fedha hizo zimeelekezwa katika huduma za Afya ya Msingi zinazosimamiwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Kuhusu msukumo mpya wa Bima ya Afya kwa Wote na Afya Kidijitali, Mchengerwa, amesema Tanzania ipo katika kipindi cha mageuzi makubwa, huku lengo kuu likiwa utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote. 

Wakati bima hiyo ikipanua ulinzi wa kifedha kwa wananchi, Mfuko wa Pamoja wa Afya unabaki kuwa mhimili wa kuhakikisha huduma bora na zenye usawa zinapatikana kwa wote.

Akizungumzia dira ya muda mrefu, amesema Tanzania inalenga kupunguza utegemezi mkubwa wa bidhaa za afya kutoka nje kwa kuwekeza katika uzalishaji wa ndani wa dawa, vifaa tiba na teknolojia za afya.

Wakati huo huo, Mabalozi wamepongeza Rais dokta Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa kwenye Sekta ya Afya, pangezi zilizotolewa na Elke Wisch, Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto-UNICEF huku Mratibu wa Wadau wa Mfuko wa Pamoja wa Afya, akimshukuru Rais Samia kwa kazi kubwa katika kuokoa vifo vya mjawazito na mtoto wakati wa kujifungua.

Hakuna maoni: