Breaking


Jumapili, 15 Machi 2026

UTABIRI WA HALI YA HEWA KWA SAA 24 ZIJAZO


 Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania imetoa utabiri wa hali ya hewa kwa saa 24 zijazo kuanzia saa 3:00 usiku wa leo Machi 15, 2026, ikieleza kuwa maeneo mengi nchini yanatarajiwa kuwa na hali ya mawingu kiasi pamoja na vipindi vya jua huku baadhi ya maeneo yakipata mvua zinazoambatana na ngurumo za radi. 

Mikoa ya kusini na nyanda za juu kusini ikiwemo Ruvuma, Mbeya, Iringa, Njombe, Songwe na Rukwa inatarajiwa kupata mvua katika maeneo machache, huku hali kama hiyo ikitarajiwa pia katika baadhi ya maeneo ya kanda ya ziwa, magharibi na katikati ya nchi.


Kwa upande wa ukanda wa pwani unaojumuisha Dar es Salaam, Tanga, Pwani pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba, hali ya mawingu kiasi inatarajiwa kutawala ikiwa na vipindi vya jua na uwezekano wa mvua katika maeneo machache. 

Upepo wa pwani unatarajiwa kuvuma kutoka Kaskazini Mashariki kwa kasi ya takribani kilomita 20 kwa saa, huku hali ya bahari ikitarajiwa kuwa na mawimbi madogo.


Kwa mujibu wa utabiri huo, viwango vya juu vya joto vitafikia nyuzi joto 32°C katika jiji la Dar es Salaam huku kiwango cha chini kikitarajiwa kuwa 24°C, wakati miji mingine kama Arusha, Dodoma na Mwanza ikitarajiwa kuwa na hali ya hewa ya wastani. 

Mamlaka hiyo imesema matarajio ya hali ya hewa kwa siku ya Jumanne Machi 17, 2026 yanaonyesha kuwepo kwa mabadiliko madogo tu ya hali ya hewa katika maeneo mengi ya nchi.


Hakuna maoni: