Breaking


Jumamosi, 21 Machi 2026

WANANCHI WATARAJIA RIPOTI YA TUME YA UCHUNGUZI KUIMARISHA AMANI, WAHIMIZA MARIDHIANO YA KITAIFA.

 

Wakati Tume iliyoundwa na Rais Dokta Samia Suluhu Hassan, kuchunguza matukio ya vurugu zilizojitokeza wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 ikikaribia kuwasilisha ripoti yake, wananchi pamoja na wadau wameeleza matarajio chanya wakiamini hatua hiyo itaimarisha amani, utulivu na mshikamano wa kitaifa.

Wananchi wengi katika maeneo mbalimbali wameiambia Uhuru fm tz kuwa wana matarajio makubwwa ya ripoti hiyo kutoa ukweli wa kina kuhusu matukio yaliyotokea.

Sambamba na hilo tume itatoa mapendekezo yatakayosaidia kujenga taifa lenye umoja na kuzuia migogoro ya aina hiyo siku zijazo.

Mmoja wa wananchi aliyezungumza na Uhuru fm tz, Shija Njile Masanja, amesema matarajio yake ni kuona haki na uwazi vikipewa kipaumbele kutokana na mapendekezo ya tume.

Naye, mchambuzi wa masuala ya Siasa na Utawala Bora Nchini, Peter Shayo, amesema tume ni hatua muhimu katika kujenga maridhiano na mwanzo mpya kati ya Watanzania, huku Mwanasiasa mkongwe nchini, akisema matarajio makubwa ni kuona mapendekezo ya tume yakitekelezwa kwa vitendo.

Kwa upande wake, kiongozi wa chama cha siasa cha NLD amesema ripoti hiyo ni fursa ya kuimarisha demokrasia na mshikamano wa kitaifa.

Aidha, wakati Taifa likisubiri ripoti hiyo kuwekwa hadharani, ni vema Watanzania kulinda amani, kudumisha utulivu na kuweka mbele maslahi ya taifa ili Tanzania iendelee kuwa mfano wa mshikamano na utulivu Barani Afrika na Dunia kwa ujumla.

Hakuna maoni: