Breaking


Alhamisi, 30 Aprili 2026

BODI YA REA YASISITIZA ULINZI WA MIUNDOMBINU YA UMEME MBEYA


Bodi ya Nishati Vijijini (REB) imeeleza kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi wa kusambaza umeme katika vitongoji 105 mkoani Mbeya, huku ikitoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika kulinda miundombinu hiyo dhidi ya vitendo vya hujuma na wizi.


Akizungumza wakati wa ziara ya ukaguzi katika Kitongoji cha Iwambi, Halmashauri ya Mbeya Vijijini, Mkurugenzi wa Bodi hiyo, Florian Haule, amesema kuwa ushiriki wa wananchi ni nguzo muhimu katika kuhakikisha huduma ya umeme inaendelea kuwa salama na endelevu. Amesisitiza kuwa vifaa vya umeme ikiwemo transfoma na nyaya vinapaswa kulindwa na jamii inayovizunguka ili kuepuka hasara na kukwamisha maendeleo.


Mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 10.9 unatekelezwa na Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO), ukiwa na lengo la kuboresha upatikanaji wa umeme vijijini na kuchochea shughuli za kiuchumi kwa wananchi.

Kwa mujibu wa Mhandisi Abdallah Mitenda kutoka ETDCO, utekelezaji wa mradi unaendelea vizuri na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwisho wa Mei 2026, mapema kuliko muda uliopangwa kwenye mkataba wa awali.

Naye Meneja wa Mradi, Mhandisi Ajuaye Jeggo, amewahimiza wananchi kukamilisha maandalizi ya miundombinu ya ndani ya nyumba zao, ikiwemo kusuka waya, ili waweze kuunganishiwa huduma ya umeme kwa gharama nafuu ya shilingi 27,000. Amebainisha kuwa jumla ya wateja 3,465 wanatarajiwa kunufaika na mradi huo, unaohusisha ufungaji wa transfoma 105 pamoja na ujenzi wa laini za umeme zenye urefu wa kilomita 210.


Awali, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Rodrick Mpogolo, ameipongeza Bodi ya Nishati Vijijini kwa juhudi zake za kusimamia utekelezaji wa miradi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), akieleza kuwa usimamizi thabiti unachangia utekelezaji wa miradi yenye ubora na yenye kuleta matokeo chanya kwa jamii.


UMUHIMU WA MRADI KWA JAMII

Mradi huu unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa umeme katika maeneo ya vijijini, kuboresha huduma za kijamii kama afya na elimu, pamoja na kukuza shughuli za kiuchumi ikiwemo biashara ndogondogo na viwanda vya kati. Ushiriki wa wananchi katika kulinda miundombinu ni hatua muhimu ya kuhakikisha uwekezaji huu unadumu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.


Hakuna maoni: