Breaking


Jumatatu, 27 Aprili 2026

KAMISHNA LUOGA AONGOZA WATAALAMU KUTOKA TANZANIA KATIKA MKUTANO WA AU KUHUSU NISHATI NA UCHUKUZI.

Wizara ya Nishati na Wizara ya Uchukuzi za Tanzania zimeshiriki katika Mkutano wa 5 wa mwaka wa Kamati Maalum ya Wataalamu ya Umoja wa Afrika kuhusu Uchukuzi na Nishati (Specialised Technical Committee (STC) on Transport and Energy), unaofanyika jijini Johannesburg, Afrika Kusini 

Ushiriki wa Tanzania kwa ngazi ya wataalamu unaongozwa na Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, aliyeongoza ujumbe wa sekta kushiriki katika majadiliano ya kimkakati yanayolenga kuimarisha maendeleo ya miundombinu ya nishati na uchukuzi barani Afrika.

Wataalamu wengine walioshiriki mkutano huo ni Mkurugenzi wa Usalama wa Usafiri na Mazingira wa Wizara ya Uchukuzi, Bi. Stella Katondo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Mohamed Salum, pamoja na wataalamu wengine kutoka katika sekta husika.

Mkutano huo wa wataalamu umeanza Aprili 27 hadi 29, 2026, ambapo unajadili masuala mbalimbali ya sekta ya nishati na uchukuzi ikiwemo kuongeza uwekezaji katika nishati jadidifu, matumizi ya gesi asilia, pamoja na kuimarisha miundombinu ya umeme wa kuvuka mipaka.

Mkutano huo utafuatiwa na kikao cha Mawaziri kitakachofanyika Aprili 30, 2026, ambapo Tanzania pia itashiriki.

Katika majadiliano hayo, nchi wanachama zinaangazia mikakati ya kuboresha upatikanaji wa nishati ya uhakika na nafuu, pamoja na kuendeleza mifumo jumuishi ya uchukuzi ikiwemo reli, barabara, anga na usafiri wa majini ili kurahisisha biashara na usafirishaji barani Afrika.

Hakuna maoni: