Staa wa hip hop duniani Kanye West ameibua gumzo jipya baada ya Serikali ya Uingereza kuanza kupitia upya uamuzi wa kumruhusu kuingia nchini humo. Hatua hiyo imekuja kufuatia mjadala mkali ulioibuka baada ya kutangazwa kuwa ndiye angekuwa kinara wa tamasha kubwa la muziki jijini London.
Mashabiki wa burudani walikuwa wakisubiri kwa hamu kumuona Ye jukwaani, lakini mambo yamechukua sura tofauti baada ya baadhi ya watu kukumbushia matamshi yake ya awali yaliyokosolewa vikali. Hali hiyo imezua presha kubwa kwa waandaaji wa tamasha hilo, huku baadhi ya wasimamizi wakijiondoa na wengine wakitaka jina lake liondolewe kabisa kwenye orodha ya wasanii.
Ikumbukwe kuwa rapa huyo aliwahi kuzua utata zaidi mwaka jana baada ya kutoa wimbo ulioleta mjadala mkubwa pamoja na kuuza bidhaa zilizoibua hisia kali kwa jamii. Ingawa baadaye aliomba radhi, bado kivuli cha matukio hayo kinaonekana kumfuata hadi sasa.
Kwa upande wao, mawaziri wa Uingereza wana mamlaka ya mwisho kuamua iwapo mtu kutoka nje ya nchi anaruhusiwa kuingia, hasa pale ambapo uwepo wake unaonekana kutokuwa na manufaa kwa umma. Wakati mjadala ukiendelea kupamba moto, macho yote sasa yako kwa serikali kuona itachukua hatua gani.
Si mara ya kwanza kwa Ye kukumbana na hali kama hii, kwani tayari aliwahi kupigwa marufuku kuingia Australia, jambo linaloonyesha namna sakata hili linavyozidi kuchanganya tasnia ya burudani duniani.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni