Kitulo Garden Marathon ni mbio za riadha zinazotarajiwa kufanyika katika Hifadhi ya Taifa ya Kitulo, wilayani Makete, Mkoani Njombe, Mei 2, 2026, zitakazohusisha maelfu ya watu kutoka ndani na nje ya nchi.
Mbio hizo zitahusisha ukimbiaji umbali wa kilometa 5, 10 na kilometa 21.1 ndani ya hifadhi ya Kitulo, yenye mandhari nzuri ya kuvutia kwa maua yenye uzuri wa kipekee, milima, maporomoko ya maji na hali ya hewa nzuri na wadudu wenye sauti ya kuvutia.
Kitulo Garden Marathon imeanzishwa na kuratibiwa na Kitulo sports, events and Promotion chini ya Mkurugenzi Mkuu, Dokta Toba Nguvila, ambaye pia ni Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, ikiratibiwa na Mony Luvanda.
Lengo likiwa ni kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta Samia Suluhu Hassan katika kuutangaza utalii wa ndani ya nchi, kama kutangaza utalii wa Kitulo na Makete, kukuza maendeleo ya kiuchumi katika eneo husika, kuhamasisha michezo na afya, kuitangaza Tanzania kimataifa, kuchangia katika maendeleo ya kijamii na kuimarisha ushirikiano.
Katika mbio hizo, kutakuwa na vitu vingi vya kuvutia ndani ya hifadhi, ambapo mbali na kukimbia pia kutakuwa na burudani mbalimbali ikiwemo muziki, ngoma za asililakini pamoja na matenti kwa ajili ya malazi ndani ya hifadhi 'full adventure'.
Mratibu wa Mbio hizo, ametoa wito kwa Watanzania wote kujitokeza kujisajili kupitia Whatsapp namba 0754 241241 kwa kuandika neno Kitulo kwa kiasi cha Sh. 40,000, ambayo itaweza kumuwezesha kupata 'T.shirt' maalumu kwa ajili ya kukimbilia, namba ya ushiriki (BIB), medali ya kushiriki ikiwa pamoja na kiingilio cha hifadhi.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni