Breaking


Jumatano, 22 Aprili 2026

KONGAMANO LA ZIWA TANGANYIKA LAZAA MATUNDA, GAVANA (DRC) ATETA NA TANTRADE KUHUSU BIASHARA NA TANZANIA

Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) zimefungua ukurasa mpya wa kuimarisha ushirikiano wa kibiashara, hatua inayolenga kuimarisha biashara ya kikanda na kuongeza uwekezaji baina ya mataifa haya mawili. 

Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Dkt. Latifa Khamis, alisisitiza kuwa TanTrade ni daraja la biashara kati ya Tanzania na mataifa ya nje, akiwakaribisha wafanyabiashara kutoka DRC kutumia fursa zilizopo nchini. Alieleza kuwa Tanzania imejipanga kutumia lango la magharibi kupitia Kigoma katika kuimarisha biashara kwenye nchi za Ushoroba wa Kati kwa kurahisisha huduma za usafirishaji na upatikanaji wa bidhaa za viwandani na vyakula ili kuongeza mchango wa sekta binafsi katika uchumi wa kikanda.

Kwa upande wake, Gavana wa Jimbo la Kivu Kusini (Bukavu), Profesa Jean-Jacques Purusi Sadiki, amewahimiza wafanyabiashara wa Tanzania kuwekeza nchini DRC, akibainisha kuwa kuna nafasi nyingi za kibiashara na uwekezaji katika sekta mbalimbali. Aliongeza kuwa serikali ya DRC itaendelea kuhakikisha mazingira salama kwa wawekezaji, ili kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kukuza biashara ya kikanda.

Aidha, Gavana ameishukuru TanTrade kwa mwaliko wa kuja kushiriki Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa SabaSaba na amesema ataambatana na wafanyabiashara wakubwa ili kupata fursa zaidi za biashara katika maonesho hayo yatakayoanza tarehe 28 Juni 2026.

Hakuna maoni: