Breaking


Jumatatu, 13 Aprili 2026

MCHEZAJI DOMINIC FRIMPONG AUAWA KWA RISASI KWENYE SHAMBULIO LA BASI LA TIMU


Tasnia ya soka nchini Ghana imekumbwa na pigo kubwa kufuatia kifo cha mchezaji wa Berekum Chelsea, Dominic Frimpong, aliyeuawa kwa kupigwa risasi baada ya basi la timu yake kushambuliwa na majambazi wenye silaha. 

Tukio hilo la kusikitisha lilitokea usiku wa Jumapili, wakati timu hiyo ikirejea nyumbani baada ya mchezo wa Ligi Kuu ya Ghana dhidi ya Samartex uliochezwa katika mji wa Samreboi, kusini mwa nchi hiyo.


Kwa mujibu wa taarifa rasmi kutoka Chama cha Soka cha Ghana, shambulio hilo lilitokea katika barabara ya Goaso kuelekea Bibiani, eneo ambalo limekuwa likiripotiwa kuwa na changamoto za kiusalama mara kwa mara. 

Inadaiwa majambazi hao waliwashambulia wachezaji na viongozi wa timu wakiwa safarini, hali iliyosababisha taharuki kubwa kabla ya tukio hilo kugeuka kuwa janga kufuatia kifo cha Frimpong.


Klabu ya Berekum Chelsea imethibitisha kifo cha mchezaji huyo aliyekuwa akicheza nafasi ya winga, huku wachezaji, benchi la ufundi na mashabiki wakibaki katika mshtuko mkubwa. 

Kifo chake kimeacha pengo kubwa ndani ya timu na tasnia nzima ya soka nchini Ghana, hasa ikizingatiwa mchango wake uwanjani na nje ya uwanja.


Tukio hili pia limeibua upya mjadala kuhusu usalama wa wachezaji na timu wanapokuwa safarini, hususan katika safari za ndani zinazofanyika kwa barabara. 

Wadau mbalimbali wa soka nchini Ghana wameanza kutoa wito kwa mamlaka husika kuchukua hatua za haraka na madhubuti kuhakikisha usalama wa timu zote, ili kuepusha matukio kama haya yasijirudie tena.


Wakati uchunguzi ukiendelea kubaini chanzo na wahusika wa shambulio hilo, familia ya marehemu, klabu ya Berekum Chelsea na mashabiki wa soka kwa ujumla wanaendelea kuomboleza kifo cha mchezaji huyo, ambaye ameondoka akiwa katika kilele cha taaluma yake ya soka.


Hakuna maoni: