Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), CPA Anthony Kasore, amewahimiza viongozi na watendaji wa vyuo vya ufundi stadi kuimarisha ushirikiano na viwanda na waajiri ili kuhakikisha mafunzo yanayotolewa yanakidhi mahitaji halisi ya soko la ajira.
Kasore ametoa kauli hiyo mkoani Kigoma wakati wa ziara yake ya siku mbili iliyoanza Aprili 9 hadi 10, 2026, akitembelea vyuo vya VETA Kigoma na VETA Buhigwe kufuatilia utekelezaji wa Mradi wa Wezesha Binti unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya VETA na Shirika la Enabel.
Kasore amesema mafanikio ya mradi huo yanategemea ushirikiano madhubuti wa wadau wote, akitaka uwekezaji uliofanyika uendelee kuleta matokeo chanya kwa muda mrefu.
“Mwalimu anapaswa kushirikiana na viwanda, kutembelea maeneo ya kazi na kuwapeleka wanafunzi kujifunza kwa vitendo ili kuongeza ufanisi wa mafunzo,” amesisitiza.
Akiwa katika ziara hiyo, amekagua karakana na kujionea maboresho ya miundombinu pamoja na vifaa vya kisasa vilivyotolewa kupitia mradi huo, akieleza kuwa hatua hiyo imeanza kuzaa matunda.
“Mradi wa Wezesha Binti umeonesha matokeo chanya kupitia uboreshaji wa miundombinu na upatikanaji wa vifaa vya kisasa vya kufundishia. Ni wajibu wetu kuvihifadhi na kuvitumia ipasavyo ili kudumisha ubora wa mafunzo,” amesema.
Ametolea mfano fani ya Uungaji na Uundaji Vyuma, akisema uwepo wa mashine za kisasa unatoa fursa kwa vijana kupata ujuzi utakaowawezesha kufanya kazi ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake, Meneja wa Mradi wa Wezesha Binti Mkoa wa Kigoma, Christine Karungi, amesema mradi huo unalenga kuwawezesha vijana, hususan wasichana na wanawake vijana, kupata ujuzi na kushiriki katika ajira na ujasiriamali huku wakizingatia utunzaji wa mazingira.
Amebainisha kuwa zaidi ya Sh. Bilioni 7.5 zimetengwa kwa ajili ya kusaidia vyuo saba vya ufundi stadi, huku shabaha ikiwa ni kunufaisha vijana 2,300.
Mradi wa Wezesha Binti ni ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Ufalme wa Ubelgiji kupitia taasisi ya Enabel, ukilenga kuwawezesha vijana wenye umri wa miaka 14 hadi 29, hususan walioko katika mazingira hatarishi, kupata elimu, ujuzi na fursa za ajira zenye staha.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni