Mwenge wa Uhuru 2026 umemaliza mbio zake katika Wilaya ya Ilala, ikiwa ni wilaya ya kwanza kuanza mbio hizo katika Mkoa wa Dar es Salaam. Katika wilaya hiyo, miradi saba yenye thamani ya shilingi 52,088,900,245.72 imepitishwa na Mwenge wa Uhuru bila hata mmoja kukataliwa.
Akizungumza na wananchi waliojitokeza kushuhudia shughuli za Mwenge, Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Wazo Mwang’onda, alisema lengo la Mwenge wa Uhuru ni kuleta matumaini, kuhamasisha amani, upendo, na kuangazia maendeleo ya taifa ndani na nje ya mipaka yake.
Aliongeza kuwa dhamira hiyo inaendelezwa na Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kufuatia misingi iliyoasisiwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Katika ziara yake wilayani Ilala, chini ya usimamizi wa Mkuu wa Wilaya, Edward Mpogolo, Mwenge umetembelea, kukagua, kuweka mawe ya msingi na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo.
Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa kitega uchumi cha DDC Kariakoo, barabara ya lami katika Mtaa wa Lindi, kisima cha Ilala Kota, kituo cha afya Mchikichini, shule mpya ya sekondari Kitunda Relini, kituo cha polisi Bonyokwa, pamoja na kikundi cha vijana “Fighter” kinachojihusisha na usafirishaji wa abiria kwa pikipiki.Leo Aprili 14, 2026, Mwenge wa Uhuru unaendelea na mbio zake katika Wilaya ya Kigamboni, ambapo utatembelea, kukagua, kuweka mawe ya msingi na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo.
Kauli mbiu ya Mwenge wa Uhuru 2026 ni: “Tanzania ni Yetu Sote, Tushikamane kwa Pamoja Kuleta Maendeleo.”




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni