Wilaya ya Ilala leo Aprili 13, 2026 imepokea Mwenge wa Uhuru kwa shamrashamra huku ukitarajiwa kuipita katika maeneo mbalimbali ukizindua na kukagua miradi ya maendeleo yenye lengo la kuboresha maisha ya wananchi.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya Mwenge huo toka kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Albert Chalamila, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amesema, Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2026, utazindua miradi yenye thamani ya shilingi Bilioni 151,822.
Amesema Ilala Katika hatua ya kuimarisha uchumi wa wananchi, Mwenge huo utazindua Mradi wa Kitega Uchumi katika eneo la Kariakoo, hatua inayotarajiwa kuongeza fursa za kipato kwa wananchi na kukuza biashara ndogondogo.
Aidha, katika sekta ya miundombinu, Mwenge utapita na kukagua ujenzi wa Barabara ya Lindi kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita 1.015, mradi unaolenga kuboresha usafiri na kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam.
Katika kuendeleza huduma za kijamii, Mwenge wa Uhuru utazindua miradi kadhaa ikiwemo kisima cha maji na kituo cha afya katika eneo la Mchikichini, hatua itakayosaidia kuboresha upatikanaji wa huduma muhimu kwa wananchi.
Sekta ya elimu nayo haitaahwa nyuma, ambapo Mwenge utazindua mradi wa shule ya sekondari Kitunda Relini, huku pia utazindua kituo cha polisi Bonyokwa kwa lengo la kuimarisha usalama wa raia na mali zao.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amewahimiza wananchi kuendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
Katika hatua nyingine, vikundi vya vijana vikiwemo Fighters vilipata nafasi ya kuonesha shughuli zao katika eneo la Segerea, ikiwa ni jitihada za kuhamasisha ushiriki wa vijana katika shughuli za kijamii na kiuchumi.
Shughuli za Mwenge zitahitimishwa katika eneo la Tabata kwa mkesha maalum uliohusisha kusomwa kwa risala, ujumbe wa Mwenge wa Uhuru 2026 pamoja na burudani mbalimbali kabla ya kilele cha shughuli hizo.
Kaulimbiu ya mwaka huu inasema: “Tanzania ni yetu sote, tushikamane kwa pamoja kuleta maendeleo,” ikisisitiza umuhimu wa umoja na ushirikiano katika kufanikisha maendeleo ya taifa.
Aidha mbio za Mwenge wa Uhuru katika Wilaya ya Ilala umeendelea kuwa chachu ya maendeleo kwa kuibua, kuzindua na kuhamasisha utekelezaji wa miradi yenye tija kwa wananchi.


Hakuna maoni:
Chapisha Maoni