Breaking


Ijumaa, 24 Aprili 2026

RAIS DKT. MWINYI ASISITIZA UBORESHAJI WA MFUMO WA VIZA KIDIGITALI NA UIMARISHAJI WA USALAMA NCHINI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameishauri Wizara ya Mambo ya Ndani kuimarisha mfumo wa utoaji wa viza kwa njia ya kidigitali ili huduma hiyo ipatikane kwa haraka kwa wageni wanaoingia nchini.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 24 Aprili 2026, alipokutana na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Patrobas Katambi, aliyefika Ikulu Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha.

Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa kwa muda mrefu kumekuwepo na tatizo la upatikanaji wa viza kupitia mfumo wa mtandao (online), jambo linalolalamikiwa na watalii wengi wanaoingia nchini na kusababisha kutumia muda mrefu kupata huduma hiyo katika viwanja vya ndege.

Amefahamisha kuwa hatua hiyo itaongeza ufanisi na kudhibiti upotevu wa fedha unaotokana na matumizi ya fedha taslimu. 

Amesisitiza kuwa kuwepo kwa mfumo wa kidigitali ni suala la lazima katika utoaji wa viza, na kuitaka Wizara kuchukua hatua za haraka kuondoa tatizo hilo.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa suala jingine linalopaswa kupewa kipaumbele na Idara ya Uhamiaji ni uwajibikaji katika viwanja vya ndege, pamoja na kuimarisha utoaji wa huduma kwa haraka kwa kuwa na nguvu kazi ya kutosha muda wote na kuwajibika kwa ufanisi zaidi.

Sambamba na hilo, Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza kwa Jeshi la Polisi kuimarisha usalama katika maeneo ya utalii ili kudhibiti matukio ya uhalifu, pamoja na kuongeza juhudi za kufanya uchunguzi wa haraka pale matukio yanapotokea na kuweka utaratibu mzuri wa utoaji wa taarifa kwa umma.

Akizungumzia suala la usalama barabarani, amesema juhudi za ziada zinahitajika kuimarisha utekelezaji wa sheria za usalama barabarani kutokana na kutofuatwa kikamilifu kwa sheria hizo, hali inayochangia ongezeko la ajali za barabarani. 

Pia amesisitiza kuimarishwa kwa juhudi za kupambana na udhalilishaji wa kijinsia, tatizo alilolieleza kuwa ni kubwa hapa nchini.

Naye Waziri wa Mambo ya Ndani, Patrobas Katambi, amemuhakikishia Rais Dkt. Mwinyi kuwa Wizara hiyo itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa utii na uaminifu, kwa kuzingatia Katiba, sheria na sera za nchi, na ameahidi kuyapokea na kuyafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa kama dira ya utekelezaji. 

Hakuna maoni: