Breaking


Alhamisi, 30 Aprili 2026

SERIKALI YASISITIZA USHIRIKI WA VIJANA KATIKA KUCHOCHEA UKUAJI WA UCHUMI


Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa vijana kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa, ikieleza kuwa kundi hilo lina nafasi kubwa katika kufanikisha ukuaji wa uchumi jumuishi na endelevu.

Akizungumza jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa kongamano la kwanza la kisayansi la vijana kuhusu masuala ya VVU/UKIMWI, afya ya uzazi, jinsia na masuala mtambuka, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Profesa Palamagamba Kabudi amesema kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inalenga kuwajengea vijana uwezo na kuwapa kipaumbele katika safari ya maendeleo.

Amesema dira hiyo inalenga kujenga taifa lenye rasilimali watu yenye elimu, ujuzi na maono, huku vijana wakipewa nafasi ya kutumia vipaji vyao katika kuleta mabadiliko chanya ya kiuchumi na kijamii.

“Vijana ni nguvu kazi muhimu katika maendeleo ya taifa. Kupitia ubunifu, ujasiriamali na uwajibikaji, wanaweza kuwa chachu ya mageuzi ya kiuchumi,” amesema Profesa Kabudi.

Serikali Kuimarisha Afya ya Jamii na Ulinzi wa Vijana

Katika hatua nyingine, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mikakati madhubuti ya kukabiliana na changamoto zinazoikumba jamii, hususan ukatili wa kijinsia na afya ya akili.

Profesa Kabudi ameeleza kuwa serikali imeanzisha madawati maalum ya ulinzi na huduma za msaada katika maeneo mbalimbali ikiwemo shule, vyuo na ngazi za jamii, ili kuhakikisha huduma hizo zinawafikia wananchi kwa urahisi na kwa wakati.

Kongamano la Vijana Latoa Fursa ya Kujifunza na Kubadilishana Mawazo

Awali, akimkaribisha mgeni rasmi, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Dkt. James Kilabuko, alieleza kuwa kongamano hilo ni jukwaa muhimu kwa vijana kujifunza, kushirikishana uzoefu na kujenga uwezo wa kukabiliana na changamoto za kiafya na kijamii.

Amesema elimu itakayopatikana kupitia kongamano hilo itasaidia kujenga jamii yenye uelewa mpana, yenye afya bora na yenye uwezo wa kufanya maamuzi sahihi kwa mustakabali wa taifa.

Kongamano hilo la siku mbili limeandaliwa na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) na linaongozwa na kaulimbiu isemayo:

“Kuunganisha Sayansi na Ubunifu katika Kukabiliana na Janga la VVU, Afya ya Uzazi na Jinsia kuelekea Dira ya Maendeleo 2050.”

Hakuna maoni: