Breaking


Jumamosi, 11 Aprili 2026

TPSF YAUNGA MKONO JUHUDI ZA SERIKALI KUELEKEA AFCON 2027

 

Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) limeeleza fahari yake kwa kuunga mkono na kuendeleza juhudi za Serikali katika maandalizi ya mashindano ya AFCON 2027. Aidha, TPSF imezipongeza wizara husika pamoja na taasisi mbalimbali, ikiwemo TISEZA, kwa uongozi thabiti na uratibu unaoendelea kuhakikisha maandalizi hayo yanafanikiwa.


Katika kuunga mkono jitihada hizo, TPSF imeandaa ziara maalum iliyowakutanisha wadau wa sekta binafsi kutoka nyanja tofauti, kwa lengo la kujionea maendeleo ya miradi na kuelewa kwa kina fursa zilizopo. Ziara hiyo ilifanyika mkoani Arusha, ambapo walitembelea pia uwanja wa AFCON Arusha, Samia Suluhu Hassan Stadium.


Kupitia maandalizi ya AFCON 2027, imeelezwa kuwa kuna fursa kubwa za uwekezaji katika sekta mbalimbali ikiwemo malazi (hospitality), usafirishaji na usimamizi wa mizigo (logistics), ujenzi, utalii, huduma za kidijitali pamoja na minyororo ya ugavi.


Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Deogratius Massawe, amesema kuwa taasisi hiyo ina mpango wa kuendeleza ziara kama hizo katika maeneo mengine yatakayokuwa mwenyeji wa mashindano hayo, ikiwemo Zanzibar na Dar es Salaam. Lengo ni kuhamasisha ushiriki mpana wa sekta binafsi na kufungua zaidi fursa za kiuchumi kwa Watanzania.



TPSF imehitimisha kwa kusisitiza kuwa AFCON 2027 siyo tu tukio la michezo, bali ni jukwaa muhimu la kukuza biashara, uwekezaji na uchumi wa taifa kwa muda mrefu.


Hakuna maoni: