Waziri wa Kilimo Daniel Chongolo ametangaza neema kwa wakulima wa Idofi, Wilaya ya Makambako, ambapo Serikai inaenda kutekeleza mradi Mkubwa wa Umwagiliaji utakaonufaisha ekari zaidi ya 1.300.
Amesema, hatua hiyo itainua uchumi hivyo ni muhimu kuunga mkono mpango wa Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji wa kutekeleza mradi huo wa ujenzi wa miundombinu ya Umwagiliaji katika skimu ya Idofi, utakaowezesha kilimo chenye tija na kufungua fursa mbalimbali za maendeleo katika eneo hilo.
Chongolo amesema hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi ya Idofi.
Amesema, Serikali imejipanga kuhakikisha wananchi wanatumia kikamilifu rasilimali zilizopo ili kujiletea maendeleo endelevu.
Amesema alibaini kuwa wananchi wengi hawalimi kwa tija licha ya kuwa na maeneo makubwa, kutokana na changamoto ya maji na miundombinu duni ya kilimo.
Hata hivyo, amewahimiza wananchi kuwa tayari kushirikiana na Serikali kwa kutoa nafasi kwa muda mfupi ili kuruhusu utekelezaji wa mradi, kabla ya kurejeshwa katika maeneo yao kwa manufaa makubwa zaidi.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Makambako, Kenneth Haule, amewahimiza wananchi kujifunza kutoka katika maeneo ambayo tayari yamenufaika na miradi ya Umwagiliaji kama vile Igomelo, Pawaga na Itipingi, ambako uzalishaji umeongezeka kwa kiasi kikubwa.
Mhandisi wa Umwagiliaji Mkoa wa Njombe, Machage Mwema, amesema wananchi watapewa umiliki wa maeneo yao ndani ya mradi huo na watakuwa na mamlaka ya kufanya maamuzi juu ya matumizi ya ardhi zao.






Hakuna maoni:
Chapisha Maoni