Mafunzo hayo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam Mei 11, 2026, yalilenga kuongeza uelewa wa masuala ya miliki ubunifu na kubadilishana uzoefu kuhusu namna bora ya kusimamia na kulinda haki hizo kupitia mfumo wa sheria.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo kwa niaba ya Jaji Kiongozi, Jaji Imani Aboud alisema kuwa elimu hiyo ni muhimu katika kuimarisha uwezo wa mahakama kushughulikia mashauri yanayohusu miliki ubunifu kwa weledi zaidi.Alieleza kuwa maamuzi yanayotolewa na mahakama yana athari kubwa ndani na nje ya nchi, kwani mara nyingi hutumika kama rejea katika mifumo mingine ya sheria, jambo linaloongeza umuhimu wa kuwa na uelewa wa kina kuhusu haki za miliki ubunifu.
Kwa upande wake, Jaji wa Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Dar es Salaam, Dkt. Cleoface Morris, alisema kuwa mashauri mengi yanayofikishwa mahakamani yanahitaji tafsiri sahihi ya sheria ili kuhakikisha haki za wabunifu, wawekezaji na wafanyabiashara zinalindwa ipasavyo.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa, amesema mafunzo hayo ni sehemu ya mpango endelevu wa taasisi hiyo wa kutoa elimu kwa wadau mbalimbali wa sekta ya sheria na biashara kuhusu umuhimu wa miliki ubunifu katika maendeleo ya uchumi wa taifa.Amesema kuwa baadhi ya hukumu zilizotolewa na mahakama tayari zimekuwa msaada mkubwa katika utekelezaji wa majukumu ya BRELA, huku akisisitiza kuwa ushirikiano kati ya taasisi za sheria na wadau wa miliki ubunifu ni muhimu katika kujenga mazingira bora ya biashara na ubunifu nchini.
BRELA imeendelea kutoa mafunzo kwa majaji, mawakili na wadau wengine wa sheria kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma, kuimarisha uelewa wa masuala ya miliki ubunifu na kuongeza ulinzi wa haki za wabunifu nchini Tanzania.



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni