Breaking


Jumamosi, 23 Mei 2026

WAZIRI MKUU AKAGUA UJENZI WA BARABARA YA MCHEPUO YA MJI WA IRINGA

Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika miradi ya kimkakati ya miundombinu ili kuboresha usafiri, kuongeza ufanisi wa uchukuzi na kufungua fursa mpya za maendeleo ya kiuchumi nchini.

Amesema Barabara ya Mchepuo ya Mji wa Iringa yenye urefu wa kilomita 7.3 itasaidia kupunguza msongamano wa magari, kuongeza biashara na kuchochea ukuaji wa mji wa Iringa.

Dkt. Nchemba amesema hayo leo Jumamosi Mei 23, 2026 wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo inayojengwa kwa kiwango cha lami mkoani Iringa. Mradi huo unaotekelezwa na kampuni ya SINOHYDRO Corporation Limited kwa usimamizi wa TANROADS kupitia kitengo cha TECU, unagharimu shilingi bilioni 41.6.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Samia Suluhu Hassan imeendelea kutekeleza miradi mikubwa ya barabara nchini kwa lengo la kuimarisha uchumi na kurahisisha huduma za usafiri na uchukuzi. Aidha, amesema barabara hiyo itakuwa suluhisho la kudumu la msongamano wa magari katika mji wa Iringa, hasa eneo la mlima wa Ipogoro lililokuwa likikumbwa na ajali na changamoto za usafiri.


Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema mradi huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kujenga barabara za mchepuo katika miji mikubwa ili kupunguza msongamano wa magari.

Hakuna maoni: