Wirtz amesema Salah ni mmoja wa wachezaji waliokaa kwa muda mrefu ndani ya klabu hiyo na anaifahamu vizuri mazingira ya timu pamoja na changamoto zake. Kutokana na uzoefu wake, Salah huwa anasema kile anachokiamini bila kuficha hisia zake, jambo ambalo Wirtz anaamini ni la kawaida katika soka la kisasa.
“Mo ameijua klabu kwa muda mrefu sana. Yeye ni mtu mkweli na huongea kile anachofikiri. Hilo linapaswa kuwa sawa. Kama mtu anataka kuzungumza, anapaswa kuwa huru kufanya hivyo,” alisema Wirtz.
Aidha, Wirtz alikiri kuwa msimu uliopita haukuwa rahisi kwa wachezaji wengi wa kikosi hicho, akiwemo Salah mwenyewe, hali iliyosababisha baadhi ya kauli au ujumbe kutafsiriwa tofauti na mashabiki pamoja na vyombo vya habari.
Kwa mujibu wa Wirtz, mjadala uliotokana na ujumbe huo uliongezwa ukubwa kuliko ulivyostahili, huku akisisitiza kuwa kwa mtazamo wake Salah hakumshambulia mtu yeyote bali alikuwa akieleza hisia zake kuhusu hali ya timu katika kipindi kigumu cha msimu.
Kauli hiyo imeendelea kuzua mjadala miongoni mwa mashabiki wa soka duniani, hasa kutokana na nafasi kubwa anayoshikilia Salah ndani ya Liverpool F.C. na mchango wake mkubwa kwa mafanikio ya timu hiyo katika miaka ya hivi karibuni.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni