Klabu ya soka ya Crystal Palace F.C. imeendelea kuweka rekodi mpya baada ya kutwaa taji lake la tatu ndani ya kipindi cha miezi 12, kufuatia ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Rayo Vallecano katika fainali ya Conference League iliyochezwa mjini Leipzig.
Shujaa wa mchezo huo alikuwa mshambuliaji wa Ufaransa, Jean-Philippe Mateta, aliyefunga bao pekee lililoihakikishia Palace ushindi na kutwaa taji lao la kwanza kabisa la mashindano ya Ulaya. Ushindi huo pia umeongeza mafanikio makubwa ya klabu hiyo baada ya kutwaa kombe la FA msimu uliopita.
Bao hilo lilipatikana dakika sita baada ya kuanza kwa kipindi cha pili, kufuatia shuti la Adam Wharton kuokolewa na kipa wa Rayo Vallecano, Augusto Batalla, kabla ya Mateta kutumia vyema mpira wa rebound na kuufunga kwa karibu.
Mateta sasa ameifikia idadi ya mabao 16 msimu huu akiwa na Crystal Palace, licha ya ripoti zilizokuwa zikimuhusisha na kujiunga na AC Milan katika dirisha la usajili la Januari kabla ya majeraha ya goti kuzuia dili hilo kukamilika.
Kocha wa Palace anayetarajiwa kuondoka klabuni humo, Oliver Glasner, ameondoka akiwa ameandika historia kubwa ndani ya miaka miwili na nusu aliyokaa Selhurst Park, baada ya kuiongoza timu hiyo kutwaa mataji ya FA Cup, Community Shield pamoja na Conference League.
Mchezo huo uliokuwa wa kwanza kwa timu zote mbili kucheza fainali ya mashindano ya Ulaya, ulianza kwa tahadhari kubwa ndani ya dimba la Red Bull Arena. Rayo Vallecano walitengeneza nafasi kadhaa kupitia Alemao na Unai Lopez, lakini Crystal Palace walionekana kuwa na hatari zaidi kuelekea mapumziko.
Katika kipindi cha pili, Yeremy Pino aliipa Rayo Vallecano matumaini ya kusawazisha baada ya kuunda nafasi kadhaa, ikiwemo mipira ya adhabu iliyogonga nyavu za pembeni mara mbili. Hata hivyo, Crystal Palace walionyesha uimara mkubwa wa safu yao ya ulinzi hadi dakika za mwisho na kufanikiwa kuandika historia mpya kwa kutwaa ushindi huo muhimu.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni