Breaking


Alhamisi, 28 Mei 2026

MOTO WATEKETEZA BWENI LA SHULE YA WASICHANA GILGIL




Shirika la Msalaba Mwekundu Kenya limethibitisha kufika eneo la tukio la moto ulioteketeza bweni katika Chuo cha Wasichana Utumishi kilichopo Gilgil, Kaunti ya Nakuru nchini Kenya, huku kukiwa na hofu ya kuwepo kwa vifo vya wanafunzi.


Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na mamlaka husika, moto huo ulianza majira ya saa saba usiku na kuripotiwa rasmi saa tisa na nusu usiku wa kuamkia Alhamisi.


Kupitia taarifa yake, Shirika la Msalaba Mwekundu Kenya limesema linaendelea kushiriki katika operesheni ya dharura ili kusaidia waathirika wa tukio hilo.


“Baada ya tukio la moto lililoripotiwa saa 3:30 usiku katika Chuo cha Wasichana Utumishi, Kaunti ya Nakuru, timu zetu zimefika eneo la tukio kusaidia shughuli za uokoaji na huduma za dharura,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.


Shirika hilo limeongeza kuwa wahudumu wa kwanza, ambulensi za EMS Kenya pamoja na wataalamu wa usaidizi wa kisaikolojia wamepelekwa eneo la tukio kusaidia wanafunzi walioathirika na familia zao.


Wakati huo huo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Bonde la Ufa, Samuel Ndanyi, amesema bado kuna wanafunzi wasiopungua kumi ambao hawajulikani walipo kufuatia tukio hilo.


“Timu za uchunguzi zinaendelea kukusanya taarifa na kuwabaini wanafunzi wote waliohusika katika tukio hili. Kuna taarifa za vifo, lakini ni muhimu kwanza familia zipewe taarifa rasmi,” amesema Ndanyi.


Shughuli za uokoaji na uchunguzi wa chanzo cha moto huo zinaendelea, huku wazazi wengi wakikusanyika nje ya shule wakitaka kupata taarifa kuhusu watoto wao. Polisi wameendelea kudhibiti eneo hilo kwa kuruhusu wazazi pekee kuingia ndani ya shule.


Baadhi ya wanafunzi waliojeruhiwa wamepelekwa katika Hospitali ya St. Joseph’s Gilgil kwa ajili ya matibabu na uchunguzi zaidi.


Mamlaka nchini Kenya zinaendelea kufuatilia hali ya tukio hilo huku wananchi wakisubiri taarifa rasmi kuhusu chanzo cha moto na idadi kamili ya walioathirika.


Hakuna maoni: