Akizungumza baada ya kutembelea mradi huo na kukagua maendeleo ya ujenzi, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, alisema kazi za ujenzi zimefikia hatua za mwisho huku sehemu kubwa ya miundombinu muhimu ikiwa imekamilika.
Alieleza kuwa mradi huo ulianza mwaka 2022 kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania, Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Mfuko wa Afrika Growing Together Fund (AGTF), ukiwa na lengo la kujenga uwanja wa kisasa unaokidhi mahitaji ya mji mkuu wa nchi.“Dodoma ni makao makuu ya nchi, hivyo ni muhimu kuwa na uwanja wa ndege wa kisasa unaoweza kuhudumia ongezeko la shughuli za kiuchumi, kiserikali na kijamii,” alisema Waziri huyo.
Kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji wa mradi, sehemu ya kwanza inayohusisha miundombinu ya msingi ya uwanja imefikia asilimia 86.73 ya utekelezaji. Aidha, sehemu ya pili inayojumuisha majengo muhimu kama jengo la abiria, mnara wa kuongozea ndege na jengo la zimamoto imefikia asilimia 75.1.Uwanja huo utakuwa miongoni mwa viwanja vikubwa nchini ukiwa na njia ya kuruka na kutua ndege yenye urefu wa kilomita 3.6 na upana wa mita 60. Pia utakuwa na maegesho makubwa ya ndege yatakayowezesha kuhudumia ndege nyingi kwa wakati mmoja.
Kuongeza Uwekezaji na Ukuaji wa UchumiSerikali inaeleza kuwa kukamilika kwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato kutafungua fursa zaidi za safari za ndani na nje ya nchi, kuongeza uwekezaji na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Dodoma na Tanzania kwa ujumla.
Jengo la abiria la uwanja huo linatarajiwa kuwa na uwezo wa kuhudumia abiria takribani milioni 1.5 kwa mwaka, jambo litakaloongeza uwezo wa jiji la Dodoma kupokea wageni, wawekezaji na watalii kutoka maeneo mbalimbali duniani.
Mbali na njia ya ndege na jengo la abiria, mradi huo pia unahusisha ujenzi wa mnara wa kisasa wa kuongozea ndege wenye urefu wa mita 56.2, jengo la zimamoto la kiwango cha kimataifa, majengo ya kuzalisha umeme pamoja na jengo la hali ya hewa lenye vifaa vya kisasa vya usimamizi wa usafiri wa anga.
Mradi wa Kimkakati kwa TaifaKwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya, alisema Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato ni miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa nchini kwa lengo la kuimarisha miundombinu na kukuza uchumi.
Alibainisha kuwa uwanja huo umejengwa kwa viwango vya kisasa vya kimataifa na umebuniwa kwa mtazamo wa muda mrefu ili uweze kupanuliwa kulingana na mahitaji yatakayojitokeza baadaye.
“Mradi huu ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha sekta ya usafiri wa anga na kuvutia uwekezaji zaidi nchini. Tunahakikisha kazi zilizobaki zinakamilika kwa wakati ili uwanja uanze kutumika kama ilivyopangwa mwezi Septemba,” alisema.
Kukamilika kwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato kunatarajiwa kuifanya Dodoma kuwa kitovu muhimu cha usafiri wa anga nchini na kuongeza ushindani wa Tanzania katika sekta ya usafiri wa anga ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni