Katika taarifa iliyotolewa Jumamosi, Wizara ya Afya ya Kenya ilisema kuwa kituo hicho kitasaidia kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa, kuwatenga wagonjwa wanaoshukiwa au kuthibitishwa kuambukizwa Ebola, pamoja na kuongeza uwezo wa kukabiliana na dharura za kiafya.
Wizara hiyo ilieleza kuwa uwekezaji huo utachangia kuimarisha usalama wa afya nchini Kenya kupitia maboresho ya maabara, miundombinu ya afya, mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa, pamoja na kuongeza utayari wa wataalamu wa afya katika kukabiliana na milipuko ya magonjwa mbalimbali.
“Uwekezaji huu utaimarisha usalama wa afya ya Kenya kwa kuboresha uwezo wa maabara, miundombinu ya afya, ufuatiliaji wa magonjwa, mifumo ya kukabiliana na dharura, na utayari wa wafanyakazi wa afya zaidi ya tishio la sasa la Ebola,” ilisema taarifa ya wizara hiyo.
Tangazo hilo limekuja siku chache baada ya mahakama nchini Kenya kutoa amri ya kusitisha kwa muda utekelezaji wa mpango wa kuanzisha kituo hicho, wakati maandalizi ya kuanza shughuli zake yakiwa katika hatua za mwisho.
Kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa kati ya Kenya na Marekani, kituo hicho chenye uwezo wa kuhudumia wagonjwa 50 kilitarajiwa kutumika kuwahudumia raia wa Marekani wanaoweza kuathiriwa na ugonjwa wa Ebola katika eneo la Afrika Mashariki na maeneo jirani.
Mpango huo umeibua mjadala kuhusu mchango wake katika kuimarisha usalama wa afya ya umma na namna utakavyotekelezwa kwa kuzingatia maslahi ya wananchi wa Kenya.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni