Mamlaka za usalama zililazimika kupeleka maelfu ya maafisa wa polisi katika maeneo mbalimbali, hususan jijini Paris, ili kudhibiti hali ya usalama baada ya baadhi ya mashabiki kufanya vurugu wakati wa kusherehekea ushindi huo.
Kwa mujibu wa taarifa za polisi, huduma za usafiri wa umma zikiwemo mabasi, treni na reli ziliathirika kutokana na machafuko hayo. Polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya watu waliokuwa wamekusanyika katikati mwa jiji, huku baadhi ya watu wakiripotiwa kujeruhiwa.
Video zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha matukio ya moto katika baadhi ya maeneo, baiskeli zikiteketea barabarani pamoja na uharibifu wa mali ikiwemo kuvunjwa kwa vioo vya baadhi ya maduka.
Eneo maarufu la Champs-Élysées lilijaa mashabiki muda mfupi baada ya PSG kutwaa ubingwa huo kupitia ushindi wa mikwaju ya penalti dhidi ya Arsenal. Aidha, mapema kabla ya mechi kumalizika, makabiliano yaliripotiwa kati ya polisi na baadhi ya mashabiki waliokuwa wakitazama mchezo kwenye skrini kubwa katika uwanja wa Parc des Princes.
Polisi wamesema magari sita, biashara kadhaa pamoja na maeneo ya kuegesha mabasi yaliharibiwa wakati wa vurugu hizo. Matukio kama hayo pia yalishuhudiwa mwaka jana baada ya PSG kushinda taji hilo, ambapo sherehe za ushindi ziligeuka kuwa machafuko.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ufaransa, Laurent Nuñez, amesema mamlaka zilikuwa zimejiandaa kwa kiwango kikubwa mwaka huu ili kukabiliana na uwezekano wa kutokea kwa vurugu zinazohusiana na sherehe za ushindi wa timu hiyo.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni