Breaking


Jumapili, 17 Mei 2026

KITUO CHA UBIA PPPC CHATOA MAFUNZO KWA MAAFISA MADAWATI YA PPP


Dar es Salaam. Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP-Centre) kimetoa mafunzo kwa maafisa wa madawati ya PPP kutoka mamlaka mbalimbali za serikali kwa lengo la kuwaimarisha katika uibuaji, uchambuzi na usimamizi wa miradi ya ubia nchini.

Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo maafisa kutoka serikali kuu, mamlaka za serikali za mitaa pamoja na wadau wa sekta binafsi ili waweze kuelewa kwa kina utekelezaji wa miradi ya PPP na majukumu yao ya kisheria.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Kitengo cha Maandalizi na Uchambuzi wa Miradi ya  PPP.  Augustino Saibull amesema kitengo hicho kina jukumu la kutoa usaidizi wa kiufundi kwa taasisi za serikali katika kuandaa maandiko ya miradi pamoja na kufanya uchambuzi wa miradi inayowasilishwa.

Amesema pia PPP-Centre hutoa mafunzo kwa taasisi za serikali na sekta binafsi kuhusu utekelezaji wa miradi ya PPP ili kuongeza uelewa na ufanisi katika utekelezaji wa miradi hiyo.

“Tumekuwa tukitoa mafunzo kwa mamlaka za serikali, serikali za mitaa pamoja na sekta binafsi ikiwemo taasisi za kifedha ili kuwajengea uwezo wa kusimamia miradi ya PPP,” alisema.

Aidha amesema kupitia Sheria ya PPP na kanuni zake, serikali imeunda vyombo mbalimbali ikiwemo madawati ya PPP na vitengo maalumu vya PPP katika mamlaka za serikali za mitaa kwa lengo la kuratibu utekelezaji wa miradi hiyo.

Ameongeza kuwa sababu kubwa ya kuendesha mafunzo hayo ni kuwakumbusha maafisa hao wajibu wao wa kisheria pamoja na kuwapa uelewa mpana wa taratibu za PPP kuanzia hatua ya uibuaji wa miradi, maandalizi, ununuzi hadi usimamizi wake.

Hakuna maoni: