Breaking


Jumatano, 20 Mei 2026

KUNENGE APONGEZA MAFANIKIO YA SEKTA YA USHIRIKA MKOA WA PWANI


Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amepongeza jitihada zinazofanywa na sekta ya ushirika kwa kuendelea kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika Mkoa wa Pwani, akisema mkoa huo umeendelea kuwa mfano wa mafanikio ya ushirika nchini.

Kunenge amesema mafanikio yanayopatikana kupitia vyama vya ushirika yamechangia kuupa Mkoa wa Pwani heshima kubwa kitaifa kutokana na utendaji mzuri wa vyama hivyo pamoja na tuzo mbalimbali vinazoendelea kupata.

Akizungumza katika Kikao cha Jukwaa la Sita la Ushirika Mkoa wa Pwani kilichofanyika katika Ukumbi wa Density, Kibaha, Mkuu huyo wa Mkoa alisema ushirika una mchango mkubwa katika kuwainua wananchi kiuchumi kupitia huduma za kifedha, uwekezaji na uboreshaji wa maisha ya wanachama.

Kikao hicho kilihusisha viongozi wa vyama vya ushirika, wanachama pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo ya ushirika kutoka ndani na nje ya Mkoa wa Pwani.

Aidha, Kunenge amewataka viongozi wa vyama vya ushirika kuhakikisha wanapunguza gharama za uendeshaji ili huduma zinazotolewa kwa wanachama ziwe nafuu zaidi, zenye tija na manufaa kwa wananchi wengi.

Pia amesisitiza umuhimu wa kuzingatia uwazi, uwajibikaji pamoja na maadili mema katika usimamizi wa vyama vya ushirika ili kuongeza imani kwa wanachama na kuendelea kukuza sekta hiyo muhimu ya uchumi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Ushirika Mkoa wa Pwani, Charles Maguye, amesema kupitia juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, Mkoa wa Pwani umeendelea kupata mafanikio makubwa katika sekta ya ushirika.

Maguye amesema mafanikio hayo ni pamoja na ongezeko la hisa na akiba za SACCOS, utoaji wa mafunzo kwa viongozi na wanachama pamoja na vyama vya ushirika vya mkoa huo kuendelea kupata tuzo mbalimbali za kitaifa kutokana na utendaji wao mzuri.

Hata hivyo, amebainisha kuwa bado kuna changamoto kadhaa zinazohitaji ufumbuzi, ikiwemo ubovu wa miundombinu ya barabara, ucheleweshaji wa malipo kwa baadhi ya SACCOS pamoja na changamoto za masoko ya mazao.

Amesema wanaushirika wanaendelea kuiomba Serikali kushirikiana nao katika kutafuta suluhisho la changamoto hizo ili sekta ya ushirika iweze kuendelea kukua na kuchangia maendeleo ya wananchi pamoja na uchumi wa taifa kwa ujumla.


Hakuna maoni: