Maafisa Habari, Itifaki, Mawasiliano na Uhusiano kutoka wizara na taasisi mbalimbali nchini wamepanda miti 2,000 katika eneo la chanzo cha maji cha Agafilo mkoani Njombe, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za taifa za uhifadhi wa mazingira na vyanzo vya maji.
Zoezi hilo limefanyika sambamba na kikao kazi cha maafisa hao kinachoendelea mkoani Njombe tangu Mei 6, 2026, kilichoandaliwa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Miti hiyo imepandwa kwa lengo la kuimarisha uhifadhi wa mazingira na kulinda vyanzo vya maji vinavyochangia utekelezaji wa mradi wa kuhakikisha wakazi wa Njombe wanapata huduma ya maji safi, salama na ya kutosha.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Habari–Maelezo, Bw. Kevin Kanje, alisema Serikali itaendelea kuhamasisha taasisi na wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za uhifadhi wa mazingira ili kuhakikisha rasilimali za maji zinaendelea kudumu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
“Tunatambua umuhimu wa mazingira katika maendeleo ya taifa letu. Upandaji wa miti hii 2,000 ni sehemu ya juhudi za kuifanya Tanzania kuwa ya kijani na salama kwa mazingira,” alisema Bw. Kanje.
Alisema maafisa habari wana wajibu mkubwa wa kuielimisha jamii kuhusu umuhimu wa utunzaji wa mazingira kupitia vyombo mbalimbali vya mawasiliano wanavyovitumia katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Kwa upande wake, Mhifadhi wa Misitu Wilaya ya Njombe kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), SCO Audatus Kashamakula, alisema miti iliyopandwa imezingatia aina zinazosaidia kulinda vyanzo vya maji na kurejesha uoto wa asili katika maeneo muhimu ya mazingira.
Alisema TFS itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali pamoja na wananchi kuhakikisha miti iliyopandwa inatunzwa ili kufikia malengo ya uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mmoja wa washiriki wa kikao kazi hicho alisema zoezi hilo limewapa nafasi ya kujifunza kwa vitendo umuhimu wa utunzaji wa mazingira na namna kila mmoja anavyoweza kushiriki kulinda rasilimali za taifa.
Zoezi hilo limeelezwa kuwa sehemu ya mshikamano wa maafisa habari katika kuunga mkono kampeni za taifa za upandaji miti, utunzaji wa mazingira na uhifadhi wa vyanzo vya maji.



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni