Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema jamii inapaswa kurejea katika misingi ya malezi ya pamoja na uwajibikaji wa kijamii ili kujenga kizazi chenye maadili, kinachoheshimu viongozi, wazazi pamoja na taasisi za jamii.
Dkt. Mwigulu amesema hayo leo Jumapili, aliposhiriki Ibada ya Pentekoste katika Kanisa Kuu la KKKT Usharika wa Iringa Mjini iliyoongozwa na Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Iringa, Dkt. Blaston Gavile.
Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za dini katika kuimarisha huduma za kijamii, malezi ya maadili na utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayogusa maisha ya wananchi.
Aidha, Waziri Mkuu amesema kuanzia mwaka 2028 Serikali itaanza rasmi utekelezaji wa elimu ya lazima ya miaka 10 kwa watoto wote wa Kitanzania kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha nne kwa lengo la kuongeza ujuzi na kuwajengea vijana uwezo wa kujitegemea.
Kwa upande wake, Askofu wa KKKT Dayosisi ya Iringa, Dkt. Blaston Gavile amepongeza kazi kubwa inayofanywa na Waziri Mkuu katika kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi pamoja na kuendelea kusimamia maendeleo ya Taifa kwa karibu.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni