Tanzania imeandika historia mpya katika sekta ya afya baada ya kuzindua rasmi huduma za Mfumo wa msaada wa kupumua nakusafisha damu nje ya mwili, ECMO (Extracorporeal Membrane Oxygenation), hatua inayotajwa kufungua ukurasa mpya wa huduma za wagonjwa mahututi nchini na katika Ukanda wa Afrika Mashariki
Akizungumza katika uzinduzi wa Kongamano hilo la Kwanza la ECMO Afrika Mashariki lililofanyika Mei 23 kwa kuandaliwa na Najmi Consultancy kwa kushirikiana na Hospitali ya Saifee Tanzania, Mratibu wa Utalii Tiba kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Asha Mahita, kwa niaba ya Wizara ya Afya, amesema Tanzania imeanza rasmi safari ya huduma za ECMO, hatua itakayochochea maendeleo ya huduma za afya za kibingwa pamoja na kukuza utalii wa tiba nchini
“Huduma ya ECMO ni teknolojia maalum inayotumika kusaidia wagonjwa wenye matatizo makubwa ya moyo na mapafu kwa muda, hususan wagonjwa wanaopata mshtuko wa moyo, nimonia kali, kusimama kwa moyo pamoja na changamoto nyingine za mfumo wa upumuaji na mzunguko wa damu” – amesema Dkt. Mahita
Aidha, kongamano hilo linaelezwa kuwa mwanzo wa safari ya mafunzo ya ECMO nchini Tanzania ambapo wataalamu wa afya kutoka maeneo mbalimbali walipata fursa ya kujifunza matumizi ya teknolojia hiyo pamoja na namna ya kuanzisha huduma zake katika hospitali za nchini. Washiriki walisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa, uwekezaji katika miundombinu ya kisasa pamoja na mafunzo endelevu ili kuhakikisha huduma hiyo inapatikana kwa ufanisi
Kwa upande wao, Wadau wa afya waliohudhuria kongamano hilo wameeleza uzinduzi wa huduma za ECMO unaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazoanza kutoa huduma za kisasa za wagonjwa mahututi katika ukanda wa Afrika, huku hatua hiyo kusaidia na kuimarisha mfumo wa afya nchini, kuongeza ubora wa huduma za matibabu na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha huduma za afya za kibingwa katika Afrika Mashariki
Wataalamu kutoka fani mbalimbali walioshiriki, wamekubaliana ECMO itaongeza uwezo wa matibabu ya wagonjwa mahututi na kuifanya Tanzania kuwa kituo cha utalii wa matibabu Afrika Mashariki, huku Washiriki wakitangaza mafunzo na programu rasmi ya ECMO yataanza hivi karibuni.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni