Breaking


Jumanne, 19 Mei 2026

SERIKALI KUANGALIA UPYA SHERIA ZA UHIFADHI NA MIPAKA YA HIFADHI-DKT. MWIGULU


Waziri Mkuu, Dokta Mwigulu Nchemba, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dokta Samia Suluhu Hassan ni Serikali inayowajibika kwa wananchi na ipo tayari kuyafanyia kazi maoni yote yaliyotolewa na Wabunge kuhusu sekta ya Maliasili na Utalii.

Waziri Mkuu, amesema hayo Bungeni jijini Dodoma wakati akitoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja zilizotolewa na wabunge katika mjadala wa kupitisha bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii, ya mwaka wa fedha 2026/2027.

Tayari, Rais Dokta Samia, ameelekeza Wizara ya Maliasili na Utalii kushirikiana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Wizara ya Katiba na Sheria kupitia upya masuala yanayohusu sekta hiyo, ikiwemo sheria namba 111 na 116.

Aidha, Waziri Mkuu, amesema Serikali imebaini kuwepo kwa changamoto katika baadhi ya sheria za uhifadhi, hususan zinazohusiana na utoaji wa adhabu ambazo kwa sasa zinafanana hata kwa makosa yenye uzito tofauti.

Katika hali ya sasa, sheria zinaweka adhabu zinazofanana kwa makosa tofauti ikiwemo mtu anayekutwa na mkaa na anayehusika na biashara haramu ya meno ya tembo, pamoja na mkulima anayelima ndani ya maeneo ya hifadhi na mtu anayejihusisha na ujangili.

Aidha, Waziri Mkuu, amesema kutokana na maelekezo ya Rais Dokta Samia, Serikali itaangalia upya sheria hizo kwa lengo la kuhakikisha zinaboresha ustawi wa wananchi ili kuwa na uhifadhi na utalii endelevu kwa manufaa ya taifa.

Hakuna maoni: