Breaking


Alhamisi, 28 Mei 2026

SERIKALI NA WADAU WAENDELEA KUIMARISHA HUDUMA ZA MAMA NA MTOTO NCHINI

Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imeendelea kuimarisha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto nchini ili kuhakikisha Tanzania inafikia malengo ya kimataifa katika sekta ya afya. Hatua hiyo inalenga kuongeza upatikanaji wa huduma bora, salama na zenye viwango kwa kina mama pamoja na watoto wachanga.

Akizungumza Mei 28, 2026 katika hafla ya kupokea na kukabidhi vifaa tiba pamoja na magari mawili kwa ajili ya kusaidia huduma za mama na mtoto katika Hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam, Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe amesema Serikali itaendelea kuwekeza zaidi katika sekta ya afya ili kuboresha huduma kwa wananchi.


Dkt. Magembe amesema Serikali imeendelea kuimarisha mazingira ya kazi kwa wahudumu wa afya pamoja na kuongeza uwezo wa wakunga ili kuhakikisha huduma za afya ya uzazi na mtoto zinapatikana kwa ubora unaohitajika katika maeneo mbalimbali nchini.


Aidha, amesema ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa maendeleo umeendelea kuleta mafanikio makubwa katika kuboresha huduma za afya ya uzazi, hususan kwa kina mama wajawazito na watoto wachanga.

Kwa upande wake, Mwakilishi kutoka Ubalozi wa Canada nchini Tanzania, Kevin Tokar amepongeza utekelezaji wa mradi huo na kuahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuimarisha huduma za ukunga nchini. Amesema huduma bora za ukunga zina mchango mkubwa katika kuokoa maisha ya mama na mtoto.

Naye Mwakilishi wa UNFPA Tanzania, Mark Bryan Schreiner amesema uwekezaji katika wakunga ni hatua muhimu ya kuhakikisha ujauzito salama pamoja na kuboresha maisha ya wanawake na watoto wachanga.

Mkunga Elizabeth Kawogo kutoka moja ya vituo vya afya vilivyonufaika na mradi huo amesema vifaa vya “Learning Corner” vimechangia kuongeza ufanisi katika mafunzo na utoaji wa huduma kwa kina mama na watoto.

Mradi wa Thamini Uzazi Salama (SMIT) ni mradi wa miaka saba unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na UNFPA Tanzania kwa ufadhili wa Global Affairs Canada. Mradi huo unalenga kuongeza idadi ya wakunga wenye ujuzi na kuboresha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto katika mikoa ya Dar es Salaam na Shinyanga.


Hakuna maoni: