Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa kushirikiana na Shirika la Usimamizi wa Mazingira na Maendeleo (EMEDO) wametangaza rasmi uzinduzi wa Tuzo za Waandishi wa Habari zinazolenga kuhamasisha elimu kuhusu hali ya hewa, tahadhari za mapema na usalama majini nchini Tanzania.
Tangazo hilo limetolewa leo wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa Mbezi Garden jijini Dar es Salaam, ambapo wadau mbalimbali walisisitiza umuhimu wa vyombo vya habari katika kuelimisha jamii kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi na majanga yanayohusiana na hali ya hewa.
Akizungumza katika mkutano huo, Afisa Uchechemuzi kutoka EMEDO, Bi. Mary Francis Mahemba, alisema kuwa wanahabari wana mchango mkubwa katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kwa wakati kuhusu tahadhari za hali ya hewa na usalama kwenye maji.
Alieleza kuwa taarifa sahihi zinaweza kusaidia kuokoa maisha, kupunguza madhara ya majanga na kuongeza uelewa wa jamii kuhusu hatua za kujikinga dhidi ya hatari mbalimbali zinazotokana na hali mbaya ya hewa.
“Waandishi wa habari ni wadau muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu tahadhari za hali ya hewa, usalama majini na hatua za kujikinga dhidi ya majanga,” alisema Bi. Mary Francis Mahemba.
MAENEO YATAKAYOSHINDANIWA KATIKA TUZO
Kwa mujibu wa waandaaji, tuzo hizo zinalenga kuhamasisha utayarishaji wa habari zenye ubora katika maeneo yafuatayo:
- Matukio ya hali mbaya ya hewa na athari zake kwa jamii;
- Tahadhari za mapema za hali ya hewa;
- Usalama wa usafiri na usafirishaji majini;
- Uzuiaji wa ajali na vifo vitokanavyo na kuzama maji;
- Ustahimilivu wa jamii dhidi ya majanga yanayohusiana na hali ya hewa.
TMA na EMEDO wameeleza kuwa tuzo hizo zitawahusisha waandishi wa habari kutoka redio, televisheni, magazeti, mitandao ya kijamii pamoja na majukwaa mbalimbali ya kidijitali nchini Tanzania.
Waandishi wa habari wanatakiwa kuwasilisha kazi zao zilizochapishwa au kurushwa hewani ndani ya kipindi cha mwaka mmoja kuanzia tarehe 1 Agosti 2025 hadi 30 Agosti 2026.
Kazi zote zinapaswa kutumwa kupitia barua pepe:
- media@meteo.go.tz
- mediahaliyahewa@gmail.com
TMA YASEMA TAHADHARI ZA MAPEMA NI MUHIMU KUOKOA MAISHA
Kwa upande wake, Meneja Masoko na Uhusiano kutoka TMA, Bi. Monica Mutoni, alisisitiza umuhimu wa matumizi ya taarifa za hali ya hewa na mifumo ya tahadhari za mapema, hasa kwa wananchi wanaotegemea shughuli za maji kama uvuvi na usafiri wa majini.
Alibainisha kuwa TMA itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha mchango wa wanahabari katika masuala ya hali ya hewa unatambuliwa na kupewa thamani inayostahili.
USHIRIKIANO WA TAASISI KATIKA KUKABILIANA NA MAJANGA
Ushirikiano kati ya TMA na EMEDO ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za umma, mashirika ya kiraia pamoja na vyombo vya habari katika kuongeza uelewa wa matumizi ya taarifa za hali ya hewa kwenye shughuli za kijamii na kiuchumi.
Kupitia tuzo hizi, wadau wanaamini kuwa jamii itaendelea kupata elimu sahihi kuhusu tahadhari za mapema, usalama majini na namna ya kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi nchini Tanzania.


Hakuna maoni:
Chapisha Maoni