Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, ameweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 220 kutoka Benaco hadi Kyaka pamoja na kituo cha kupoza umeme cha Benaco, ambao utaunganisha Mkoa wa Kagera kwenye Gridi ya Taifa, hatua itakayomaliza changamoto ya kukatika kwa umeme katika wilaya za mkoa huo.
Waziri Ndejembi ameweka jiwe la msingi Mei 9,2026,wilayani Ngara mkoani Kagera, ambapo amemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi huo kuukamilisha ndani ya miezi 24 kama mkataba unavyoelekeza.
“Tunachotarajia ni kuona ndani ya miezi 24 Mkoa wa Kagera umeunganishwa kwenye Gridi ya Taifa na changamoto za umeme zilizowasolishwa naMbunge wa Ngara ziwe historia kwa wananchi hawa,” amesema Ndejembi.
Akizungumza na wananchi, Waziri Ndejembi amesema kuwa mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Benaco hadi Kyaka unalenga kuunganisha Mkoa wa Kagera kwenye Gridi ya Taifa na kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika wakati wote.
Ameeleza kuwa Mkoa wa Kagera kwa muda mrefu umekuwa ukitegemea umeme kutoka nchi jirani, hivyo kupitia mradi huo Mkoa wa Kagera utaunganishwa moja kwa moja na Gridi ya Taifa, hatua itakayoongeza uhakika wa nishati na kuimarisha shughuli za kiuchumi na kijamii.
Aidha, Waziri Ndejembi amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kutoa fedha za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati na kueleza kuwa Wizara itaendelea kusimamia kwa ukaribu utekelezaji wa miradi hiyo ili kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa uhakika wakati wote.
Katika hatua nyingine, amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO kuhakikisha ndani ya mwezi mmoja inapatikana transfoma yenye uwezo mkubwa pamoja na kuendelea kufanya marekebisho katika njia za kusafirishia umeme ili kuhakikisha wananchi wa Wilaya ya Ngara wanapata umeme wa uhakika katika kipindi wanachosubiri mradi huo ukamilike





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni