Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limekutana na mawakala wa meli pamoja na wadau wa sekta ya usafirishaji jijini Dar es Salaam kujadili changamoto ya ucheleweshaji wa ushushaji wa makasha tupu katika bandari kavu, hali inayochangia msongamano na kupunguza ufanisi wa huduma za usafirishaji nchini.
Kikao hicho kilichofanyika Mei 8, 2026, kililenga kuweka mikakati ya pamoja ya kuhakikisha shughuli za usafirishaji wa mizigo zinaendelea kwa ufanisi huku Bandari ya Dar es Salaam ikiendelea kutoa huduma bora kwa wafanyabiashara wa ndani na nchi jirani zinazotumia bandari hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Meneja Udhibiti wa Huduma ya Usafiri Meli wa TASAC, Bi. Fatuma Masenene, alisema ongezeko la makasha tupu limekuwa likisababisha baadhi ya malori kuchelewa kushusha makasha hayo katika maeneo maalum yaliyotengwa, jambo linalochangia msongamano kwenye bandari kavu na kuathiri mtiririko wa usafirishaji wa mizigo.Alieleza kuwa TASAC inaendelea kufuatilia kwa karibu huduma za usafirishaji wa majini pamoja na shughuli za mawakala wa meli ili kuhakikisha changamoto zinazojitokeza zinapatiwa ufumbuzi wa haraka na wa kudumu.
Kwa upande wao, mawakala wa meli walieleza kuwa changamoto ya ucheleweshaji wa ushushaji wa makasha tupu inachangiwa na msongamano wa magari barabarani, muda mrefu wa usafirishaji wa makasha bandarini pamoja na changamoto za miundombinu kutokana na kuongezeka kwa idadi ya magari yanayobeba makasha hayo.Katika kikao hicho, wadau walikubaliana kuweka mikakati mbalimbali ya kuboresha hali hiyo. Baadhi ya hatua zilizokubaliwa ni pamoja na kuhakikisha makasha tupu yanapakiwa kwa asilimia 100 kulingana na mipango ya mawakala wa meli, kuruhusu matumizi ya baadhi ya barabara maalum nyakati za usiku kwa usafirishaji wa makasha tupu, pamoja na kutumia bandari kavu ya Kwala kuhifadhi makasha hayo kabla ya kusafirishwa kwa njia ya treni kuelekea bandarini.
TASAC imeeleza kuwa itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya usafirishaji ili kuhakikisha changamoto zinazotokana na ongezeko la mizigo zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu, hatua itakayosaidia kuongeza ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam na kuboresha huduma za usafirishaji nchini.



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni