Breaking


Jumatatu, 25 Mei 2026

TAHADHARI YA BARIDI NA VUMBI KIPUPWE 2026: WANANCHI WATAKIWA KUCHUKUA HATUA ZA KIAFYA



Wananchi wametakiwa kuchukua hatua stahiki za kiafya ili kujikinga na athari zinazoweza kusababishwa na hali ya hewa ya baridi na vumbi katika kipindi cha msimu wa kipupwe kinachotarajiwa kuanza kuanzia Juni hadi Agosti 2026. Tahadhari hiyo inalenga kusaidia jamii kujilinda dhidi ya changamoto mbalimbali za kiafya zinazoweza kujitokeza kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa katika kipindi hicho.

Akizungumza wakati wa utoaji wa utabiri wa msimu wa kipupwe 2026, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, Dkt. Ladislaus Chang’a, amesema msimu huo unatarajiwa kuwa na hali ya joto la chini, upepo mkali pamoja na vumbi katika baadhi ya maeneo ya nchi. Amesema hali hiyo inaweza kuongeza uwezekano wa magonjwa ya njia ya hewa, mafua na changamoto nyingine za kiafya kwa wananchi, hususan watoto, wazee na watu wenye matatizo ya kiafya ya muda mrefu.

Dkt. Chang’a ameongeza kuwa ni muhimu kwa wananchi kuchukua tahadhari ikiwemo kuvaa mavazi ya kujikinga na baridi, kutumia vifaa vya kujikinga dhidi ya vumbi pamoja na kuhakikisha mazingira yanabaki safi ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza katika kipindi hicho cha kipupwe.


Aidha, amewahimiza wananchi na wadau mbalimbali kufuatilia kwa karibu taarifa za utabiri wa hali ya hewa zinazotolewa na TMA ili kusaidia kupanga shughuli zao za kila siku kwa usalama na ufanisi zaidi. Amesisitiza kuwa matumizi ya taarifa za hali ya hewa ni nyenzo muhimu katika kulinda afya, mazingira pamoja na shughuli za kijamii na kiuchumi nchini.

Hakuna maoni: