Breaking


Alhamisi, 21 Mei 2026

TANESCO YAENDELEA KUWAELIMISHA WANAOFANYA SHUGHULI ZA KIUCHUMI KWENYE MIUNDOMBINU YA UMEME


Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeendelea kuwasisitiza wananchi wanaofanya shughuli zao za kiuchumi katika miundombinu ya umeme kuondoka katika maeneo hayo kwa hiari, kwa kuwa wanahatarisha usalama wa maisha na mali zao.

Akizungumza katika muendelezo wa zoezi la kukagua miundombinu ya umeme katika eneo la Mbagala Zakhem jijini Dar es Salaam, Msimamizi Msaidizi wa Njia Kuu za Kusafirisha Umeme Mkoa wa Dar es Salaam, Nicholaus Kivelege, amesema TANESCO inafanya jitihada za makusudi kutoa elimu kuhusu athari za kuendelea kufanya shughuli za kiuchumi chini ya njia kubwa za kusafirisha umeme katika maeneo mbalimbali nchini.

Amesema licha ya jitihada hizo, bado baadhi ya wananchi wanaendelea kufanya shughuli hizo, hivyo amewaomba viongozi wa serikali za mitaa katika maeneo husika kuongeza nguvu ya kutoa elimu kuhusu madhara yanayoweza kujitokeza kwa wananchi wanapofanya shughuli zao katika miundombinu ya umeme.

Baadhi ya wananchi, akiwemo Zahali Maulidi wa maeneo ya Mbagala, licha ya kufahamu kuwa kufanya shughuli chini ya miundombinu ya umeme ni hatari, wameiomba Serikali kuangalia namna ya kuwatafutia maeneo mengine ya kufanyia kazi zao ili waweze kuondoka katika maeneo hatarishi.

Haya yamejiri wakati TANESCO ikiendelea na mkakati wa kutoa elimu kuhusu athari za kufanya shughuli za kiuchumi katika miundombinu ya umeme, ili wananchi waweze kuondoka wenyewe kwa hiari kwa ajili ya usalama wa maisha yao.

Hakuna maoni: