Hayo yamebainishwa katika ripoti mpya ya Baraza la Usafiri na Utalii Duniani, World Travel & Tourism Council, ijulikanayo kama Travel and Tourism Economic Impact 2025, iliyowasilishwa katika mkutano wa kimataifa unaofanyika ndani ya meli ya kitalii ya Crystal Cruises iliyowasili katika Bandari ya Alexandria nchini Misri leo Mei 9, 2026.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, sekta ya utalii imeendelea kuwa mhimili mkubwa wa uchumi duniani kwa kuchangia asilimia 10.3 ya pato la dunia mwaka 2025, sawa na Dola za Kimarekani Trilioni 11.7. Ripoti hiyo pia inatabiri mchango huo kuongezeka hadi kufikia Trilioni 16 mwaka 2035 huku ajira zikiongezeka kutoka watu milioni 371 hadi milioni 471 ndani ya kipindi hicho.Mtendaji Mkuu wa WTTC, Gloria Guevara, amesema sekta ya utalii ina mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi na maisha ya wananchi kuliko sekta nyingi duniani, hivyo serikali zinapaswa kuendelea kuipa kipaumbele.
Kwa upande wa Afrika, ripoti hiyo imezitaja Afrika Kusini na Tanzania kuwa vinara wa kuvutia uwekezaji mkubwa katika sekta ya utalii, huku Afrika Kusini ikiongoza kwa asilimia 7.7 na Tanzania ikifuatia kwa asilimia 7.4, viwango vilivyo juu ya wastani wa dunia wa asilimia 3.8.Aidha, Tanzania, Afrika Kusini pamoja na Kenya zimeendelea kufanya vizuri katika mapato yatokanayo na matumizi ya watalii wanaonunua bidhaa mbalimbali na kuzisafirisha nje ya nchi.
Katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Tanzania, Hassan Abbasi, alikutana na viongozi wa WTTC ambapo walijadili namna ya kuongeza mchango wa sekta ya utalii katika kukuza uchumi na ajira kwa Watanzania.
Kwa upande mwingine, viongozi wa zamani duniani akiwemo Mauricio Macri, Felipe Calderón na Matteo Renzi walieleza jinsi nchi zao zilivyofanikiwa kukuza uchumi baada ya kuipa sekta ya utalii umuhimu mkubwa.Viongozi hao wamezitaka serikali duniani kuendelea kuwekeza zaidi katika utalii wakieleza kuwa sekta hiyo ni chanzo muhimu cha ajira, mapato ya taifa na maendeleo ya jamii.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni